Mkataba wa mabomu ya mtawanyiko kutiwa saini Oslo
3 Desemba 2008Kulingana na takwimu jumla ya watu laki moja wamefanywa vilema na mabomu hayo tangu mwaka 1965.
Makubaliano hayo yalifikiwa mjini Dublin mwezi Mei mwaka huu na mkataba wenyewe unapiga marufuku utengenezaji,usafirishaji na ulimbikizaji wa mabomu ya aina yoyote ya mtawanyiko.Kadhalika unatoa wito kwa nchi shirika kuyasaidia mataifa na raia wanaoathiriwa na mabomu hayo.
Tathmini zinaonyesha kuwa wengi ya watu wanaoathirika ni raia wa kawaida.Shirika hilo linayaleta pamoja mashirika yapatayo 300 yasiyo ya kiserikali.Steve Goose mmoja ya wenyekiti wa Shirika la Kupambana na matumizi ya mabomu ya mtawanyiko CCM anaafiki kuwa hatua zimepigwa ila kibarua ndio mwanzo kimeanza
''Tumefanikiwa kufanya jambo kubwa hapa ambalo ni mchanganyiko wa sheria za kurejesha maisha ya raia katika hali ya kawaida vilevile masuala ya haki za binadamu pamoja na hatua za kibinadamu jambo litakalobadilisha maisha ya waathiriwa.Hata hivyo ndio mwanzo kibarua kimeanza.''
Mkataba huo uliofikiwa mwezi Mei na mataifa 107 mjini Dublin utaanza kutekelezwa baada ya kipindi cha miezi sita kufuatia idhini ya mataifa 30 kabla ya kuwasilishwa katika Umoja wa Mataifa ili mataifa yaliyosalia kupata fursa ya kuuidhinisha.Makubaliano hayo kadhalika yanazilazimu nchi zilizotia saini kusafisha maeneo yaliyoathirika na mabomu hayo katika kipindi cha miaka 10 pamoja na kuharibu mabomu yenyewe yaliyohifadhiwa katika kipindi cha miaka 8.
Wawakilishi kutoka mataifa 115 wanahudhuria kikao cha leo. Mfano wa hivi karibuni ni kwenye eneo la Ossetia Kusini na Abkhazia wakati wa vita kati ya Urusi na Georgia.Maafisa wa Shirika la Kutetea haki za Binadamu Human Rights Watch walishudia maovu yaliyotokea wakati huo.Mark Hiznay ni afisa wa Utafiti wa ngazi za juu katika Kitengo cha silaha kwenye Shirika la Human Rights Watch anasisitiza kuwa athari za mabomu hayo hujirudia kila yanapotumika.
''Hali hii inayojirudia rudia inaonyesha kuwa hatua mwafaka ni kuwa na mkataba maalum unaopiga marufuku matumizi ya silaha hizi kama athari zake zilivyoshuhudiwa nchini Georgia.''
Mabomu hayo yanasambazwa kwa kudondoshwa kutoka ndegeni au kufyatuliwa kwa bunduki kisha yanatawanyika kama vipande vidogovidogo vilivyo na urefu wa nchi tatu hivi.Mengi ya mabomu hayo hushindwa kulipuka na kuishia ardhini jambo linalohatarisha wakazi wa eneo husika.
Zaidi ya robo ya waathirika hao ni watoto wanaoyadhania mabomu hayo kuwa makopo au vitu vya kuchezea.Nchi ya Laos imeathirika zaidi na mabomu ya kutawanyika kote ulimwenguni.Mwaka 1964 hadi '73 Jeshi la angani la Marekani lilidondosha mabomu milioni 260 ya kutawanyika nchini humo.
Hata hivyo mataifa makubwa yanayotengeza na kutumia mabomu hayo yanapinga mkataba huo wa Oslo kadhalika hatua ya kuutia saini.
Mataifa hayo yanajumuisha Marekani,Urusi,Uchina,Israel.India na Pakistan.Mataifa 18 kati ya 26 wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya mataifa ya magharibi NATO yameahidi kutia saini mkataba huo wa Oslo.Ufaransa,Uingereza na Ujerumani zitakazowakilishwa na mawaziri wao wa mambo ya kigeni kwenye kikao cha leo nazo pia zimeridhia kutia saini mkataba huo.