Urusi yajiondoa katika mkataba wa nafaka
18 Julai 2023Mkataba huo umefikia kikomo baada ya Urusi kujiondoa na kutahadharisha kwamba haiwezi kuhakikisha usalama wa meli zitakazokuwa zinasafirisha nafaka katika bahari hiyo nyeusi.
Urusi yasema huenda ikarudi katika mkataba huo matakwa yake yakitimizwa
Umoja wa Mataifa umesema hatua hiyo ni pigo kwa watu walio na mahitaji kote duniani. Urusi imesema iwapo matakwa kuhusiana na usafirishaji wa nafaka na mbolea zake yatatimizwa, basi itatafakari kurudi katika mkataba huo wa Bahari Nyeusi.
Umoja wa Mataifa wasema makubaliano yake na Urusi pia yamefikia mwisho
Lakini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, makubaliano rasmi ya Umoja wa Mataifa yaliyokuwa na lengo la kusaidia usafirishaji wa bidhaa za Urusi, yamefikia mwisho pia. Mkataba huo wa usafirishaji wa nafaka ulifikiwa mwaka jana chini ya usimamizi wa Uturuki na Umoja wa Mataifa kusaidia kukabiliana na mzozo wa chakula uliokuwa unaikumba dunia.