1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya waitaka Afrika kusaidia mzozo wa wahamiaji

Admin.WagnerD11 Novemba 2015

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanajaribu kuelekeza mazungumzo yao juu hatua za pamoja na bara la Afrika kukabiliana na mgogoro wa wakimbizi, wakati ambapo Slovenia imekuchukua uamuzi wa peke yake wa kufunga mpaka wake.

https://p.dw.com/p/1H40w
21.08.2015 DW Themenwoche Themenbild EU Europa Flagge
Bendera ya Umoja wa Ulaya

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanapanga kupendekeza kwa viongozi wenzao wa Afrika kiasi cha hadi yuro bilioni 3.6 kama msaada ili nchi hizo kwa upande wake zihusike katika kukabiliana na mgogoro wa wakimbizi wanaomimika kuingia nchi za Ulaya.

Mkutano huo wa aina yake unaowakusanya viongozi 50 kutoka mabara hayo mawili unaonesha mwelekeo mpya katika nia ya Umoja wa Ulaya ya kuwa na mkakati wa kushirikiana katika kupambana na mgogoro huo mkubwa ambao haujapata kutokea tangu vita vya pilivya dunia.Hata hivyo hatua iliychukuliwa na Slovenia ambayo ni mwanachama wa Umoja huo wa Ulaya ya kufunga mpaka wake inaonesha kwa mara nyingine kuhusu kuwepo mgawanyiko mkubwa ndani ya Umoja huo kuhusiana na jinsi ya kuushughulikia mgogoro huo.

Jeshi la nchi hiyo lilianza hii leo kuweka senyeng'e katika mpaka wa nchi hiyo na Croatia.Baada ya Hungary kufunga mpaka wake mwezi uliopita Slovenia imejikuta kuwa njia kubwa katika eneo hilo la Balkan ya maelfu ya wakimbizi wanaomiminika kutokea Ugiriki kila siku wakitumia njia hatari ya kuvuka bahari kutoka Uturuki.

Afrika kupatiwa dola bilioni 3.6

Frankreich Straßburg Europaparlament Donald Tusk
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Donald TuskPicha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

Warasimu mjini Brusssles ambao wametia msukumo wa kufanyika mkutano huu wa Malta wanapinga hatua za kufungwa mipaka wakisema ni hatua inayochangia tu kuwafanya wakimbizi watafute njia nyingine na wakati huohuo inahujumu juhudi za kupatikana suluhisho la pamoja.

Kwahivyo katika mkutano huo wa siku mbili Umoja wa Ulaya unataka kuwashawishi viongozi wa nchi za Afrika kukubali kuchukua dola bilioni 3.6 kwa sharti kwamba zitakuwa tayari kuwapokea wahamiaji wanaozikimbia nchi za bara hilo kutokana na hali ngumu ya kiuchum.Hata hivyo hadi sasa nchi hizo za kiafrika zinaonesha kutokuwa tayari kuingia kwenye mwafaka huo kwa kuhofia kupoteza mabilioni ya dolla zinazoingia kwenye nchi hizo kupitia fedha zinazotumwa na wanachi wao wanaofanya kazi nchi za nje.

Nchi za Ulaya zinalenga hasa kuimarisha ushirikiano wake na nchi za Afrika kuwalinda wakimbizi,kuwarudisha nyumbani wahamiaji wa mara kwa mara pamoja na kukomesha biashara ya kuwapitisha kimagendo wakimbizi hao wakati pia ikiwapa nafasi waafrika kutanua njia za kisheria za uhamiaji. Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Donald Tusk fedha zitakazotolewa kwa Afrika zitasaidia kuzifanya pande hizo mbili Afrika na Ulaya kushirikiana kuweka mustakabali mzuri kwa watu wa Afrika katika wakati ambapo vijana barani humo wamekuwa mara nyingi wanajikuta wakilazimika kuchagua kati ya kubakia bila ajira au kuingia kwenye makundi ya siasa kali.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman