Mkutano juu ya Syria wafanyika Iran
9 Agosti 2012Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Ali Akbar Salehi, ameeleza kwamba nchi yake inajaribu kufufua baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa katika mpango wa amani uliopendekezwa na Kofi Annan. Salehi alieleza kwamba kati ya nchi 12 na 13 kutoka Asia, Afrika na Amerika ya Kusini zitashiriki katika mkutano huo lakini hakutaja ni nchi gani. Nchi chache zilizopelekewa mwaliko zimeshasema kwamba hazitaweza kutuma wawakilishi katika mkutano huo. Kuwait ambayo pia imetumiwa mwaliko, imekataa kushiriki, Lebanon imeeleza kwamba haitoweza kushiriki kwa sababu ya masharti ya sera ya uhusiano wake na Syria.
Naye waziri wa mambo ya nje wa Algeria, ametangaza kusikitika kushindwa kushiriki kwenye mkutano wa leo kwa sababu ya kuwa na shughuli nyingi. Hata hivyo atawakilishwa na naibu wake. Urusi imekubali pia kuuhudhuria mkutano wa leo utakaofanyika katika mji mkuu wa Iran, Tehran. Katika tamko lililotolewa hapo jana, wizara ya mambo ya nje ya Urusi, imesema kwamba nchi hiyo itawakilishwa na balozi wake wa Iran. Urusi imeahidi kuiwekea shinikizo Syria ili mapigano yanayoendelea nchini humo yaweze kusitishwa.
Vita mjini Aleppo vyaendelea
Shirika la kutetea haki za binadamu Syria lenye makao yake makuu London, Uingereza, limeripoti kwamba baadhi ya mitaa ya mji wa Aleppo, ambao ni mji mkuu wa kibiashara wa Syria, ilishambuliwa kwa mabomu usiku wa kiamkia leo. Mamia ya wanajeshi, vifaru vitatu na magari ya kijeshi yaliwasili Aleppo leo alfajiri. Kwa mujibu wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu, watu wasiopungua 22 wameuwawa nchini Syria hii leo, tisa kati yao wakiwa raia wa kawaida. Hapo jana, idadi ya watu waliopoteza maisha yao kutokana na machafuko yanayoendelea ilikuwa si chini ya 167.
Idadi ya watu wanaoikimbia Syria inaongezeka siku hadi siku. Hadi sasa inakadiriwa kwamba raia 276,000 wameshaihama nchi yao na kukimbilia nchi jirani za Jordan, Uturuki na Lebanon. Andrew Harper ni afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi, UNHCR na alisema: "Kwa bahati mbaya hatufahamu idadi ya Wasyria watakaoingia Jordan kila siku na hili ndilo suala gumu. Kila siku tunaweka mahema zaidi na yote yanajaa, hivi ni vita visivyokoma." Ili kuwahudumia wakimbizi waliopo kwenye mpaka kati ya Jordan na Syria, Ufaransa leo imetuma ndege ikiwa na madaktari, madawa na vifaa vya matibabu.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman