Mkutano kuhusu mabomu ya mtawanyiko wafanyika New Zealand
18 Februari 2008Mkutano unaojadili marufuku ya kutumia mabomu aina ya kishada unaanza leo nchini New Zealand.
Wajumbe kutoka nchi zaidi ya 120 wamekusanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Wellington, kwa mazungumzo yanayolenga kuunda mkataba wa kimataifa utakaopiga marufuku mabomu mfano wa kishada.
Mkataba huo utakaopendekezwa utalenga kuanzisha mfumo unaonuiwa kuwasaidia manusura wa mashambulio ya mabomu hayo, kuondoa mabomu kutoka ardhini ambayo bado hayajalipuka na kuharibu shehena za mabomu hayo.
Mazungumzo ya kutafuta mkataba huo yalianzishwa mwaka jana na Austria, Ireland, Mexico, New Zealand, Peru, Vatican na Norway kwenye mkutano uliofanyika mjini Oslo nchini Norway.
Mikutano ya juma hili ni ya mwisho kabla mashauriano ya kidiplomasia yaliyopangwa kufanyika mwezi Mei mwaka huu nchini Ireland.
Zaidi ya nusu ya nchi zote 76 duniani zinazorundika mabomu aina ya kishada, zinashiriki katika mkutano wa mjini Wellington, pamoja na idadi kubwa ya nchi zinazoyatengeneza mabomu hayo.