1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano mkuu wa Chama cha SPD cha Ujerumani

Miraji Othman13 Novemba 2009

Chama cha SPD cha Ujerumani kinajizatiti upya

https://p.dw.com/p/KWUW
Mkuu mpya wa Chama cha SPD cha Ujerumani, Sigmar GabrielPicha: AP

Kiongozi wa Chama cha Social Democratic, SPD, hapa Ujerumani, na ambaye anaacha wadhifa huo, Franz Münterfering, ametoa mwito kwa chama chake kianze kujijenga upya pamoja na kujiaamini baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba mwaka huu. Wakati huo huo, katika ripoti yake mbele ya mkutano mkuu wa chama unaofanyika mjini Dresden, alikubali kwamba kulifanyika makosa. Alisema maafa iliopata chama hicho katika uchaguzi wa Septemba yalikuwa ya kujitakia.

Franz Münterfering alisema kushindwa kwa chama cha SPD katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba lazima kumewatikisa wanachama. Alisema wapinzani wa kisiasa wa chama chake inafaa watambuwe sasa kwamba SPD hakitakuwa chama kidogo na kubakia kinalalamika tu, kama vile kimeonewa. Alisema:

" Chama cha SPD kimekuwa kidogo, lakini fikra ya demokrasia ya kijamii haijawa ndogo, wala haijafikia ukomo wake. Demokrasia inasonga mbele, Chama cha SPD kitabakia. Sisi ni watu tunaoweza kuendesha mapambano, na tuko tayari kuendesha mapambano. Tutarejea, marafiki."

Katika hotuba zilizotolewa mkutanoni, wajumbe kadhaa walitaka uchunguzi wa kina ufanywe kuhusu kushindwa kukubwa kwa chama chao katika uchaguzi uliopita. Chama cha SPD tangu mwaka 1998 sio tu kimepoteza wapiga kura milioni kumi, lakini pia thuluthi moja ya wanachama wake. Mkuu wa wabunge wa chama cha SPD, Frank-Walter Steinmeier, aliitathmini hotuba ya Franz Münterfering kuwa ni uchunguzi na tathmini yenye kutoka moyoni.

Bwana Münterfering alisema matokeo ya kupata SPD asilimia 23 ya kura katika uchaguzi wa Septemba 27 hayawezi kuelezewa kuwa ni kwenda juu na chini kwa kawaida kwa chama hicho, lakini ukubwa wa hasara chama hicho ilichopata ni wa kutisha. Alisema katika kampeni ya uchaguzi huo, chama cha SPD kiliregea kabisa kusema wazi pamoja na nani na nini au vipi tutayafikia yale tunayopigania. Aliashiria mafanikio kadhaa yaliopatikana kutokana na wakati ambapo chama cha Social Democratic kilikuwa kinaendesha serekali., lakini alikiri kwamba kuna mambo yaliokwenda kombo. Na hali hiyo imeonekana, kwa sehemu , na matokeo ya uchaguzi.

Wakati huo huo, Franz Münterfering alikionya chama chake kisije na majibu ya kuondoa njiani tu, majibu ya juu juu, majibu rahisi ya kukasirika, au yale yanayojisifu juu ya enzi ya zamani ya SPD, au majibu yenye kukosa moyo wa ujasiri.

Kuhusu lawama kwamba wakati yeye alipokuwa waziri wa kazi, kutokana na makubaliano ya kuunda serekali ya mseto hapo mwaka 2005, alipelekea kupitishwa sheria ya wafanya kazi kustaafu wakiwa na umri wa miaka 67, Bwana Münterfering alikumbusha kwamba jambo hilo lilipitishwa kwa kauli moja na mkutano mkuu wa Chama cha SPD. Alisema ni wazi kwamba uamuzi huo utekelezwe. Pia Münterfering aliyatetea marekebisho yaliofanywa katika soko la ajira wakati wa serekali ya Kansela Gerhard Schroader. Alisema vita dhidi ya umaskini miongoni mwa watoto sharti yake ni kwamba watu wawe na ajira. Yeyote anayetaka kuzuwia umaskini miongoni mwa wazee inambidi pia aone kwamba Ujerumani ni nchi yenye mishahara mikubwa, kwani mishahara midogo inapelekea wazee kuwa maskini. Aliionya serekali ya sasa ya mseto ya vyama vya CDU/CSU na FDP dhidi ya kupunguza hifadhi wanaoyopewa wafanya kazi kutofukuzwa kwa urahisi makazini, akitaka pia mtindo wa waajiri na vyama vya wafanya kazi kuamua masuala ya viwandani ubakie na pia pande hizo mbili ziwe huru kushauriana juu ya mishara na shuruti za kazi.

Mkutano mkuu huu wa SPD, utakaodumu hadi jumapili ijayo, utachagua kiongozi mpya na kamati yake kuu. Sigmar Gabriel, mwenye umri wa miaka 50, anapigania nafasi hiyo bila ya kuwa na mpinzani.

Naye Andrea Nahles, mwenye umri wa miaka 39, anapigania, bila ya kupigwa, kuwa katibu mkuu. Alisema kabla ya mkutano:

" Watu wote wana hamu, kwani huu ni mkutano mkuu muhimu ambao umeambatana na mabadiliko katika uongozi, mabadiliko ya kizazi. Lakini watu wote wana hakika kwamba tutakuwa na majadiliano ya kina, lakini majadiliano hayo yatabakia yenye kutengeneza mambo."

Chama cha SPD imekuwa kikidhibitiwa sana na bawa la Ki-Conservative mnamo mwongo mmoja uliopita, lakini bawa la kushoto limepata sauti tena baada ya kushindwa chama hicho uchaguzi mkuu wa Septemba.

Mwandishi: Bettina Marx/Miraji Othman/ZR

Mhariri: Mohammed Abdulrahman