1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa 39 wa Davos juu ya uchumi wa dunia unaanza leo

Miraji Othman27 Januari 2009

Kofi Annan: matatizo ya walala hoi duniani yasisahauliwe kuzungumziwa huko Davos

https://p.dw.com/p/GhM0
Mfanya kazi anafanya matayarisho ya mwisho katika jukwaa kabla ya kuanza mkutano wa Davos, UswissiPicha: AP

Wanasiasa wa dunia wanatazamiwa kuweko Uswissi leo kuhudhuria jukwa la 39 la Uchumi wa Dunia ambapo kiini cha majadiliano kinatarajiwa kitahusu mizozo ya kifedha na kiuchumi inayoendelea hivi sasa duniani. Wakuu wa nchi 40, mara mbili ya wale waliohudhuria mwaka jana, ni miongoni mwa watu mashuhuri watakaokuweko katika mkusanyiko huo wa kila mwaka na unaofanyika katika mji wa mapumziko na ulio maarufu kwa matembezi katika theluji, Davos.

Schweiz Wirtschaft Weltwirtschaftsforum in Davos Landschaft
Mandhari ya mji wa Davos ilivyofunikwa na thelujiPicha: picture-alliance/ dpa

Lakini wakuu kadhaa wa viwanda hawatakuweko Davos, kwa vile wameshapoteza kazi zao katika miezi ya karibuni kutokana na mzozo wa kifedha na kiuchumi ulioikumba sasa dunia. Mkutano huu unafanyika kabla ya mkutano wa kilele wa kundi la nchi 20 zenye uchumi mkubwa duniani huko Washington mwezi wa April. Kati ya watu 2,500 watakaoshiriki Davos, karibu asilimia 60 watatokea katika mashirika ya kibiashara duniani. Wengine wanaotazamiwa kuhudhuria ni kansela Angela Merkel wa Ujerumani, rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, na makamo wa rais wa zamani, All Gore. Serekali ya sasa ya Marekani itawakilishwa na Valerie Jarret, mshauri wa rais Barack Obama.

Naye katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alisema kwamba matatizo ya kiuchumi ya dunia hayawezi kuruhusiwa yagubike matatizo mengine yalio muhimu, kama vile kuwalinda wanadamu na mabadiliko ya hali ya hewa duniani na kuwalisha walio na njaa. Katika mahojiano aliofanyiwa kabla ya mkutano huo wa Davos, Kofi Annan alilaani mapigano ya karibuni yaliofanyika Gaza, kuwa yanachukiza, na akasema kwamba uharamia unaofanwa karibu na pwani ya Somalia ni onyo jingine katika kuyaachia mizozo inayotokota kuwa mikubwa zaidi. Mwenyekiti hyuo mashirika wa mkutano wa Davos alisema watu milioni mia moja wanaosumbuliwa na njaa ni mada muhimu kama zile zinazoangaliwa kupatiwa ufumbuzi. Wakala za misaada ya kiutu zinakisia kwamba mzozo wa sasa wa chakula duniani utasababisha watu zaidi ya milioni mia moja kuwa katika njaa, hivyo kuzidisha jumla ya watu kama hao kufikia bilioni moja.

Kofi Annan alisema anakubali kwamba mfumo wa fedha ufanywe uwe sawa, na bila ya mikopo kutolewa kupitia mfumo huo, kufufuka uchumi kutakuwa kwa polepole mno, lakini watu pia waangalie mambo kwa upana zaidi. Malalamiko kutokana na uhaba wa vyakula mwaka jana yalileta hali ya kukosekana utulivu katika baadhi ya nchi, na jambo hilo linaweza likawafanya watu walio maskini wajihisi wanatumbukia zaidi katika hali duni, huku mabilioni kwa mabilioni ya dola yanaingizwa katika mabenki ya nchi tajiri.

Kofi Annan alisema viongozi wa dunia wanahitaji kuchukuwa tahadhari na kuhakikisha kwamba mazungumzo juu ya kuurekebisha uchumi pia yanatilia maanani wasiwasi wa watu kutaka kubakia na nafasi zao za kazi, kupata chakula na kuwa na afya njema. Katibu mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Mataifa alisema matatizo yatatuliwe kwa namna ambayo kwamba risala itapelekwa kwa walala hoi, maskini na walio dhaifu kwamba matatizo yao ni muhimu pia.

Kofi Annan alisema kuna maeneo katika dunia ambako mizozo ama inasahauliwa au inaoonekana imeendelea kwa muda mrefu mno hata hamna kitu kinachoweza kufanywa kuitatua. Alisema Walimwengu wasiiachie mizozo hiyo ikawa sugu.

Pia alisema kwamba mashambulio yaliofanywa na Israel karibuni huko Gaza yametoa haja ya kupatikana kwa haraka suluhisho la kuwa na dola mbili ili kuwawezesha Wa-Israeli na Wapalastina waishi kwa amani. Alishauri kwamba pande zote katika mzozo huo, kikwemo chama cha Hamas, zinahitaji kualikwa kwenye meza ya mashauriano ili kuutanzuwa mzozo huo wa siku nyingi, tena kwa njia ilio wazi.

Der ehemalige Präsident Wladimir Putin spricht erstmals als neuer Regierungschef in Duma in Moskau
Picha: AP

Waziri mkuu wa Russia, Vladimir Putin, amepangiwa kuufungua mkutano huu wa leo wa Jukwaa la Davos.