1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa G7 wamalizika kwa kukemea China, Urusi, Iran

6 Mei 2021

Kundi la nchi saba tajiri ulimwenguni limekamilisha mkutano wake wa kwanza wa ana kwa ana katika zaidi ya miaka miwili, likiishutumu China kwa ukiukaji wa haki za binaadamu na ukandamizaji dhidi ya wapigania demokrasia

https://p.dw.com/p/3t1GU
Weltspiegel | UK G7 Treffen London
Picha: Stefan Rousseau/REUTERS

Mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka taifa mwenyeji Uingereza, pamoja na Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Canada na Japan pia wametoa wito kwa Iran kuwaachia huru raia wa kigeni na walio na uraia wa nchi mbili waliosema kuwa wanazuiliwa kiholela katika magereza ya Iran.

Wametishia kuliwekea vikwazo vipya jeshi la Myanmar ambalo lilifanya mapinduzi Februari mosi. Walijadili pia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na jinsi ya kujikwamua baada ya janga la corona.

Soma pia: China yatawala siku ya pili ya mkutano wa G7

Mataifa hayo yameahidi msaada wa kifedha kwa mpango wa kugawana chanjo wa Covax. Kundi hilo tayari limeahidi Zaidi ya dola bilioni 10.7.

Lakini hakukuwa na tangazo la haraka kuhusu ufadhili mpya wa kuimarisha upatikanaji mkubwa wa chanjo, licha ya miito inayorudiwa kwa G7 kuongeza juhudi za kuzisaidia nchi maskini.

Watetezi wa haki walilitaka Kundi la G7 kuimarisha juhudi za kupambana na ukosefu wa usawa katika vita dhidi ya janga la corona, wakati nchi za Magharibi zikizidisha kampeni zao za utoaji chanjo na kufungua shughuli za kiuchumi.

Soma zaidi: Mataifa ya G7 yaungana kujadili vitisho vya ulimwengu 

Mara tu baada ya mkutano huo kumalizika, Serikali ya Rais wa Marekani Joe Biden ikatangaza kuunga mkono msamaha wa kimataifa kwa ulinzi wa hati miliki za chanjo za Covid-19, hatua inayotoa matumaini kwa mataifa maskini ambayo yanakumbwa na changamoto ya kupata dozi za chanjo hizo za kuokoa maisha. Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Katherine Tai alisema kuwa wakati haki miliki za uvumbuzi ni muhimu, Marekani inaunga mkono msamaha kwa ulinzi huo wa chanjo za Covid-19 ili kumaliza janga hilo.

Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ameutaja uamuzi huo wa Marekani kuwa wa "kihistoria" na unaashiria tukio kubwa katika vita dhidi ya COVID19.

Wameitaka China kuheshimu majukumu yake chini ya sheria ya kimataifa na kitaifa. Wanadiplomasia hao waliikemea Urusi kwa tabia zake za uchokozi kwa kupeleka wanajeshi kwenye mpaka wa Ukraine, vitendo vibaya vya mitandao na usambazaji wa habari za kupotosha.

AFP