Mkutano wa kimataifa wa kiusalama waliofunguliwa Munich
14 Februari 2020Mkutano wa kimataifa wa kiusalama uliofunguliwa leo mjini Munich hapa Ujerumani umejikita hasa kuhusu maswala yanayotishia ulimwenguni. Marais na viongozi wa serikali wanatarajiwa pia kujadili kuhusu maadili ya kidemokrasia, vita nchini Syria, Libya na kwenye maeneo ya Sahel huko magharibi mwa Afrika.
Kwenye kikao kilichotangulia ufunguzi wa mkutano huo wa kiusalama, mmoja wa wasimamizi wake amekumbusha kwamba vita vya Darfur nchini Sudan miaka 17 iliyopita vilitokana na mabadiliko ya tabianchi na baadaye kusababisha vifo vya watu laki tatu. Vita hiyo vilihujumu mazingira ya Sudan na kuwalazimisha watu milioni mbili kuishi kwenye makambi ya wakimbizi.
Leo hii mabadiliko ya tabianchi yanasababisha kuenea kwa mizozo kwenye jimbo la Sahel, hali ambayo inaleta wasiwasi, alisema Tom Middendorp, kiongozi wa zamani wa jeshi la Uholanzi:
''Katika bara la Afrika, watu wengi wanalazimishwa kuondoka katika maeneo yao kutokana na kiangazi. Wakulima na wafugaji wamelazimishwa kuhamia maeneo mengine. Hali hii inayapa fursa makundi ya wahalifu kutekeleza visa vya uhalifu.''
Licha ya taarifa za kutisha, lakini viongozi wa dunia wanaonekana kutojali kinachoendelea, alisema waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry, ambaye amewaomba viongozi wa nchi tajiri kuchukuwa hatua muafaka na kuongeza jitihada kuhusu tatizo la mabadiliko ya tabianchi.
"Mataifa ishirini yenye uchumi mkubwa dunia, G20, yanazalisha jumla asilimia 85 ya gesi ya sumu, na hayajali kwamba nchi ndogo barani Afrika na kwengineko ulimwenguni zinatuangalia", aliendelea kusema Kerry.
Umoja wa Ulaya umesema umekuwa ukitekeleza ahadi zake na umewekeza jumla ya euro biloni nane kwa ajili ya amani, usalama na maendeleo ya kudumu kwenye jimbo la Sahel toka mwaka wa 2014. Lakini fedha hizo zote hazijabadili chochote katika kukuendelea kuwepo na ugaidi kwenye eneo hilo la Afrika Magharibi.
Ban Ki-Moon, aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema inachukiza kutofikia makubaliano kuhusu maswala ya kimataifa na mabadilko ya tabianchi, na nchi zenye nguvu zinaudharau Umoja wa Mataifa.
"Ikiwa mtauchezea Umoja wa Mataifa, nafikiri umoja huo utakuwa hauna nguvu tena, na hilo sio jawabu. Nafikiri mnatakiwa kuupa nguvu umoja huo," alisema Ban Kin Moon.
Mkutano huo wa kiusalama wa Munich, umehudhuriwa na wajumbe zaidi ya mia tano wakiwemo marais 35 kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Mwandishi: Saleh Mwanamilongo
Mhariri : Mohamed Khelef