Mkutano wa mazingira wa Warsaw wakumbwa na mivutano
22 Novemba 2013Wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa yakiwemo Oxfam,Green Peace International,Action Aid na mengine waliokuwa wamevalia fulana zilizoandikwa wachafuzi wa mazingira zungumzeni tutembee waliondoka kutoka meza ya mazungumzo katika hatua inayoonekana kutoa msukumo kwa serikali kuchukua hatua madhubuti zitakazodhibiti athari za tabia nchi.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la Oxfam Winnie Byanyima ameliambia shirika la habari la IPS kuwa walijiondoa kwenye mazungumzo hayo ya jana kwasababu hakuna hatua zozote zinazopigwa kuhusu masuala makuu waliyotarajia mkutano huo wa Umoja wa Mtaifa ungeyashughulikia huku ukitarajiwa kufikia ukingoni mwishoni mwa wiki baada ya kuwepo kwa siku kumi.
Byanyima amesema maandamano yao katika mkutano wa Warsaw ni kuzizundua serikali, hasa za nchi tajiri kuwa hazijiendeshi vizuri kuhusiana na masuala ya mabadiliko ya hewa na watawashurutisha kupitia sauti za wananchi wao.
Wanaharakati wakerwa na kujikokota kwa serikali
Mashirika yasiyo ya serikali yalitarajia kusikia matangazo kutoka nchi zilizostawi kuwa zitaunda mfumo wa ufadhili wa miradi ya kupunguza utoaji wa gesi inayochafua mazingira lakini hilo halionekani kufanyika huku mkutano huo ukikamilika Jumapili hii..
Hii inakuja siku moja baada ya wajumbe wa nchi 133 zinazoendelea kuondoka kutoka meza ya mazungumzo kupinga kusitasita kwa nchi zilizostawi kuafikiana kuhusu makubaliano ya kukabiliana na tabia nchi utakaofidia nchi zinazokumbwa na maafa.
Nchi nyingi zinazostawi zinajaribu na kushindwa kukidhi mahitaji na haki za raia wake.Kulingana na mchakato wa umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi,mkutano wa Warsaw kimsingi ni wa kupanga kwa ajili ya kongamano litakaloandaliwa Lima nchini Peru mwaka ujao, na mkutano mkuu wa mwaka 2015 nchini Ufaransa na hivyo hakukutarajiwa kuwa na matangazo makuu kutoka serikali husika.
Uchafuzi wa mazingira bado kupatiwa ufumbuzi
Mashirika yayiso ya serikali katika mkutano huo wa Warsaw yanasema yalitarajia kuwepo jitihada za kasi za kuafikia upunguzaji wa gesi inayochafua mazingira kabla ya mkutano wa Lima mwaka ujao lakini wanachoshuhudia ni serikali kujikokota kuhusiana na suala hilo kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Umoja wa Ulaya umejitolea kupunguza kutolewa kwa gesi chafu katika nchi wanachama kwa asilimia 30 iwapo tu nchi nyingine zinazotoa gesi kwa kiwango kikubwa pia zitajitolea kufanya hivyo.
Ripoti iliyotolewa na benki ya dunia katika mkutano huo wa Warsaw inaonya kuwa athari na maafa yanayotokana na mabadiliko hasi ya hewa inazidi kuongezeka.
Ripoti hiyo inasema licha ya kuwa nchi zote duniani zimeathirika na mabadiliko ya hewa,ni nchi zinazostawi ndizo zinaumia zaidi hasa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.
Huku maafa na majanga katika nchi hizo zinazoendelea yakigharimu zaidi ya dola bilioni 200 kila mwaka katika kipindi cha muongo mmoja uliopita ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka ya 80 ambapo iligharimu bilioni 50 tu kwa mwaka kufidia maafa.
Mwandishi: Caro Robi/IPS
Mhariri: Yusuf Saumu