1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Munich na hatma ya mgogoro wa Syria

2 Februari 2013

Maafisa wa Marekani, Urusi na Umoja wa Mataifa na kiongozi wa upinzani nchini Syria watahudhuria mkutano wa mwaka wa usalama mjini Munich leo(02.02.2013 kujaribu kufufua juhudi za kumaliza vita vya nchini Syria.

https://p.dw.com/p/17Wuz
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujermani Guido Westerwelle akiwasili na Rais wa Muungano wa taifa wa Syria Sheikh Moaz Al-Khatib kwa ajili ya Mkutano wa kimataifa wa usalama mjini Munich.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujermani Guido Westerwelle akiwasili na Rais wa Muungano wa taifa wa Syria Sheikh Moaz Al-Khatib kwa ajili ya Mkutano wa kimataifa wa usalama mjini Munich.Picha: Reuters

Hata hivyo utawala mjini Moscow na Umoja Mataifa walipuuza madai ya upinzani nchini Syria, kuwa kiongozi wake atafanya mkutano wa pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov, makamu wa rais wa Marekani Joe Biden na mjumbe wa kimataifa wa amani katika mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi mjini Munich. Brahimi ambaye alisema alipanga kufanya mikutano na Biden na Lavrov kandoni mwa mkutano wa mjini Munich, aliuambia mkutano huo jana Ijumaa(01.02.2013) kuwa ana mashaka juu ya kupatikana kwa suluhu la mapema la mgogoro wa Syria.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwa na makamu wa rais wa Marekani Joe Biden mjini Berlin.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwa na makamu wa rais wa Marekani Joe Biden mjini Berlin.Picha: Getty Images

"Nafahamu zaidi juu ya ugumu, juu ya kuzidi kuharibiwa kwa nchi hiyo kila siku, kuliko ninavyofahamu juu ya suluhisho," alisema wakati akizungumza katika mkutano wa pamoja akiwa pamoja na kiongozi wa upinzani, rais wa muungano wa kitaifa Moaz Al-Khatib. Lakini mwanachama wa ngazi ya juu wa muungano huo, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa Urusi inaweza kuwa inaanza kulegeza msimamo juu ya kukutana na Al-Khatib, baada ya kiongozi huyo kusema yuko tayari kufanya mazungumzo na serikali ya rais Bashar al-Assad.

Chanzo cha kidiplomasia kutoka Urusi hakikuondoa uwezekano wa mkutano huo kufanyika mara moja wakati wa mkutano wa leo(02.02.2013) mjini Munich. Kama itatokea, itakuwa mara ya kwanza kwa Marekani na Urusi, ambazo zimekuwa zikisigana juu ya endapo Assad anaweza kuwa na nafasi katika serikali ya mpito, zitakuwa zimekaa pamoja na upinzani.

Tumaini la mwisho

Afisa wa Umoja wa Mataifa na mwanadiplomasia mwandamizi wa Urusi walisema hakuna mipango kwa wote kukutana pamoja. "Mjumbe wa Umoja wa Mataifa hashiriki katika mazungumzo yoyote ya pande tatu," alisema afisa wa Umoja wa Mataifa mjini Munich. Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Gennady Gatilov alisema Lavrov hakupangiwa kushiriki mazungumzo yaliyopanuliwa. Alisema ripoti za vyombo vya habari kuhusu mkutano mjini Munich unaowahusisha Lavrov-Biden-Brahimi na muakilishi wa upinzani nchini Syria Al-Khatib haziendani na hali halisi.

Brahimi alisema si watu wa Syria, au mataifa jirani yaliyo na uwezo wa kutafuta njia ya kukomesha mgogoro huo. Alisema matumaini yamebaki kwa jumuiya ya kimataifa, na kuongeza kuwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo limegawanyika juu ya Syria ndiyo linaweza kutafuta suluhisho. "Nyinyi ndiyo rufaa ya mwisho," aliuambia mkutano huo. "Tafadhali fanyeni kazi yenu."

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle akiwa na mjumbe wa kimataifa wa amani katika mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi mjini Munich Ijumaa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle akiwa na mjumbe wa kimataifa wa amani katika mgogoro wa Syria Lakhdar Brahimi mjini Munich Ijumaa.Picha: picture alliance / AP Photo

Urusi ambayo ndiyo muuzaji mkuu wa silaha kwa Syria, imezuia maazimio matatu ya baraza la uslama kuhusu mgogoro huo wa miezi 22, na ambao umekwisha gharimu maisha ya watu 66,000. Al-Khatib alikumbana na upinzani mkali baada ya kukiuka msimamo uliyowekwa na upinzani kwa kusema kuwa yuko radhi kukaa na maafisa wa serikali ya Syria kujadili kipindi cha mpito, kama wafungwa wa kisiasa waliokamatwa tangu kuanza kwa uasi wataachiwa huru, bila Assad kukaa pembeni.

Alisema jana Ijumaa mjini Munich kuwa kama hilo linahitajika ili kukomesha umwagikaji damu, na kwa sharti kuwa wafungwa wanaachiwa, "tuko tayari kukaa kwenye meza ya mazungumzo na utawala." Brahimi aliliambia baraza la usalama wiki hii kuwa anaamini kuwa makubaliano ya kimataifa yaliyofikiwa mjini Geneva mwaka jana, ambayo kwa maksudi hayakutoa msimamo wa wazi kuhusu nafasi ya Assad huko mbele, yalieleweka kwa kiasi kikubwa, kumaanisha kuwa rais huyo hatokuwa na nafasi katika kipindi cha mpito.

Mkakati wa amani au vita

Kamati ya uongozi ya muungano yenye wajumbe 12 ilikutana hadi saa 11 alfajiri siku ya Ijumaa na kumuagiza Al-Khatib kutojibu mapendekezo yoyote yanayotolewa kwake mjini Munich bila kushauriana nao kwanza. Muundo wa muungano huo unaodhibitiwa na Waislamu wenye msimamo mkali, uliyoundwa kwa msaada wa mataifa ya magharibi na kiarabu mwezi Desemba, unamfanya Al-Khatib, mhadhiri wa madhehebu ya sunni kutoka mjini Damascus, wa kwanza miongoni mwa wajumbe walio sawa na kiongozi wa moja kwa moja.

Chanzo kutoka upinzani kilisema visu vilitolea kwa Al-Khatib kutoka kwa Waislamu wenye msimamo mkali katika kamati ya utawala na kutoka baraza la taifa la Syria baada ya matamshi yake, ambayo Kamal al-Labwani, kiongozi asiyeegemea dini na mfungwa wa kisiasa wa muda mrefu, alisema yanavunja morali ya uasi.

Al-Khatib alijitetea kuwa alihamasika kutokana na masaibu ya wafungwa, wengi wao wakiwa katika magereza ya chini ya ardhi, na kubainisha wazi kuwa bado anaamini Assad na washirika wake laazima waondoke. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani aliyemaliza muda wake Hillary Clinton aliwasihi washirika wa Assad, Iran na Urusi siku ya Alhamisi kufikiria tena misimamo yao, akisema kuwa mgogoro huo bado unaweza kusambaa nje ya mipaka yake. Zaidi ya Wasyria 700,000 wamekimbilia mataifa jirani.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere akifungua mkutano wa usalama mjini Munich Ijumaa wiki hii.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere akifungua mkutano wa usalama mjini Munich Ijumaa wiki hii.Picha: Reuters

Hali nchini Mali

Mkutano wa mjini Munich utajadili pia hali nchini Mali, wakati ambapo rais wa ufransa Francois Hollande anatarajiwa kuwasili nchini humo leo Jumamosi, kuwapa motisha wanajeshi wake na kufanya mazungumzo na rais wa muda wa nchi hiyo Diancounda Traore. Akifungua mkutano wa mjini Munich jana Ijumaa, waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas De Maziere alionya kuwa nchi itahitaji msaada wa muda mrefu ili kushughulikia mgogoro wake. "Uingiliaji kijeshi ndiyo mwanzo tu wa mchakato mrefu wa kutafuta suluhisho lakudumula mgogoro huo," alisema De Maziere.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Leon Panetta, alisema majeshi ya Ufaransa yalifanikiwa kuwafurusha waasi wa Kislamu haraka kuliko Marekani ilivyotarajia, lakini akaongeza kuwa changamoto iliyopo ni kuhakikisha kuwa usalama huo unaendelezwa bila kutumia rasilimali nyingi, na hatimaye kuweza kuondoka na kukabidhi majukumu ya usalama kwa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, dpae, afpe, ape
Mhariri. Sekione Kitojo