Mkutano wa usalama kufanyika mjini Munich
5 Februari 2012Hali isiyoeleweka kuhusiana na hali ya baadaye ya mashariki ya kati na athari za mzozo wa kifedha katika bara la Ulaya ni masuala ambayo yanaonekana kuwa yatatawala mada kuu za mkutano wa usalama unaofanyika mjini Munich hapa Ujerumani, wakati maafisa wa ngazi ya juu wa usalama na ulinzi duniani wanakusanyika mjini humo leo, kuhudhuria mkutano huo utakaodumu kwa muda wa siku tano.
Mkutano wa usalama wa Munich ambao , sasa unaingia katika mwaka wake wa 48, unawaleta pamoja maafisa kutoka mataifa zaidi ya 70 duniani, ambao ni pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton na waziri wa ulinzi wa Marekani Leon Panetta, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov , waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maiziere, waziri wa mambo ya kigeni wa ufaransa Alain Juppe, na mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya Chatherine Ashton.
Umaarufu wa mkutano huu
Umashuhuri wa mkutano huu ni kwamba huu ni mkusanyiko wa maafisa wa ngazi za juu ambapo wanaweza kuzungumzia masuala ya kisera katika hali ambayo si rasmi.
Mkusanyiko huo mwaka huu unakuja wakati wanadiplomasia wa mataifa ya magharibi wanajaribu kuzuwia upinzani wa Urusi dhidi ya azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa lenye lengo la kuzuwia ghasia na mauaji nchini Syria.
Wanadiplomasia wakizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwasababu mazungumzo ya Alhamis katika umoja wa mataifa yalikuwa si rasmi, wamesema suala kuu linaendelea kuwa lugha ambayo wawakilishi wa mataifa ya magharibi wanatafsiri kuwa inaunga mkono mpango wa amani wa mataifa ya umoja wa Kiarabu, ambao unamtaka rais wa Syria Bashar al-Assad kuachia madaraka, wakati Urusi imesema itapinga azimio lolote ambalo linaweza kutafsiriwa kuwa linatoa wito wa mabadiliko ya utawala.
Hali pana ya sintofahamu kuhusiana na mwelekeo wa mashariki ya kati baada ya mwaka wa misukosuko itazungumziwa na maafisa kama waziri mkuu wa Qatar na Tunisia, na waziri wa mambo ya kigeni wa Misri na Uturuki.
Suala la Iran linasumbua
Mtayarishaji wa mkutano huo Wolfgang Ischinger amesema kuwa Iran bado ni suala linalosumbua.
Ni matumaini yangu kuwa hatutakuwa katika hali , ambayo uwezekano pekee katika sera ya vikwazo, itakuwa ni sera ya kuelekea katika vita. Hii itakuwa kufilisika kisiasa na kidiplomasia. Nafikiri , tunapaswa kufikiria kwa kina , ni uwezekano gani ni bora zaidi , ama kuimarisha sera za vikwazo ama kuchukua msimamo wa sera za udhibiti, kama ilivyofanyika hapo zamani dhidi ya iliyokuwa Urusi ya zamani.
Hadi mapema wiki hii , hakuna ujumbe ulioorodheshwa kutoka Iran, lakini Iran mara nyingi imetuma wawakilishi wake katika dakika za mwisho. Miaka miwili iliyopita waziri wa wakati huo wa mambo ya kigeni nchini Iran Manouchehr Mottaki alijitokeza katika juhudi za kuzima miito wakati huo kutoka Marekani , Uingereza na ufaransa kuiwekea nchi hiyo vikwazo zaidi.Urusi, China na India ambazo zinatumia kwa wingi mafuta kutoka Iran , zinaweza kupambana na miito mwaka huu katika mkutano huo ya kutaka zijiunge na vikwazo dhidi ya kununua mafuta ya Iran kama ilivyokubaliwa na mataifa ya umoja wa ulaya wiki iliyopita, hatua ambayo itaanza kufanyakazi Julai mwaka huu.
Mwandishi: Sekione Kitojo/APE
Mhariri: Hamidou Oummilkheir