1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa Vienna kuyanusuru makubaliano ya nuklea ya Iran

Oumilkheir Hamidou
6 Julai 2018

((Mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka mataifa matano makubwa duniani wanakutana mjini Vienna, Austria wakipania kuitanabahisha Iran isijitoe katika makubaliano ya mwaka 2015 kuhusu mradi wake wa nyuklia.

https://p.dw.com/p/30vsR
Österreich Flagge Iran vor UN-Gebäude
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Zak

 

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje kutoka mataifa matano makubwa wanakutana na mwenzao wa Iran mjini Vienna kwa lengo la kusaka njia za kuyanusuru makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2015 pamoja na Tehran baada ya Marekani kujitoa.

Mkutano wa leo kati ya Iran, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Urusi na China utazingatia mapendekezo ya kuyanusuru makubaliano hayo yanayojulikana kwa jina "Mpango wa  Mkakati wa Pamoja" - uliolengwa kuizuwia Iran isitengeneze silaha za nyuklia.

Mwezi Mei, Rais Donald Trump wa Marekani alibatilisha makubalianao hayo yaliyofikiwa na mtangulizi wake, akihoji hayatoshi na hayazingatii hofu za Marekani na washirika wake ikiwa ni pamoja na ushawishi wa kijeshi wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati na mradi wa Iran wa kutengeneza makombora ya masafa marefu.

Rais Hassan Rohani akizungumza na kansela Kurz wa Austria
Rais Hassan Rohani akizungumza na kansela Kurz wa AustriaPicha: Getty Images/S. Gallup

Iran inatishia pia kujitoa katika makubaliano hayo

Rais Hassan Rohani wa Iran alisema mapema wiki hii angependelea kuyanusuru makubaliano  licha ya kujitoa Marekani, ikiwa lakini mataifa matano makubwa yaliyosalia yanaweza kutoa hakikisho kwamba Iran haitajikuta ikitengwa kiuchumi kutokana na vikwazo ambavyo Marekani imeamua kuvifufua.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema nchi yake pamoja na China wanapendelea kuona makubaliano yaliyofikiwa pamoja na Iran yananusurika. Kwa mujibu wa shirika la habari la RIA, Waziri Lavrov amesema hayo baada ya mazungumzo yake pamoja na mwenzake wa China, Wang Yi, mjini Vienna.

 

Mazungumzo ya kuyanusu makubalino ya mradi wa nuklea yaliyohudhuriwa na mwakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa ulaya bibi Federica Mogherini, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Javad Zarif,Ufaransa Le Drian,Ujerumani Heiko Maas na Uingereza  Boris Johnson
Mazungumzo ya kuyanusu makubalino ya mradi wa nuklea yaliyohudhuriwa na mwakilishi mkuu wa siasa ya nje wa Umoja wa ulaya bibi Federica Mogherini, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Javad Zarif,Ufaransa Le Drian,Ujerumani Heiko Maas na Uingereza Boris Johnson Picha: picture-alliance/Photoshot

Duru zaidi za mazungumzo zitahitajika

Ufaransa kwa upande wake inahisi mataifa ya Magharibi hayatoweza kutoa mapendekezo ya kiuchumi kuunusuru mradi wa nyuklia wa Iran kabla ya Novemba inayokuja. Hayo yametangazwa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian mbele ya maripota wa kituo cha matangazo cha RTL, kabla ya kuelekea Vienna.

Hoja kama hizo zimetolewa pia na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Heiko Maas. Akizungumza na waandishi habari kabla ya mazungumzo pamoja na mawaziri wenzake mjini Vienna, Heiko Maas amesema "hawatoweza kufidia kila kitu kitakachoathirika kwa kujitoa makampuni nchini Iran." Anasema haamini kama maridhiano yanaweza kufikiwa leo na kwamba pengine duru zaidi za mazungumzo zitahitajika.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa/AP/

Mhariri: Mohammed Khelef