Mkutano wa WTO warefushwa ili kufikia maelewano
15 Juni 2022Mkutano huo wa mawaziri wa biashara katika makao makuu ya WTO jijini Geneva ulitarajiwa kukamilika leo, huku shirika hilo la biashara duniani likitaraji kusaini mikataba ya kihistoria na kuthibitisha kuwa bado lina jukumu la kuchangia katika kupambana na changamoto kubwa za ulimwengu.
Lakini Mkuu wa WTO Ngozi Okonjo-Iweala, ambaye ameuweka uongozi wake katika ahadi ya kuliamsha shirika hilo lililokuwa limesinzia, amesema inaonekana masuala tata yaliyobaki yanaweza kutatuliwa kama mawaziri hao wataendelea kuyajadili. Mkutano huo ni wa kwanza wa ngazi ya mawaziri kuandaliwa na WTO baada ya karibu miaka mitano. Shirika hilo la kimataifa huchukua tu maamuzi kupitia maelewano miongoni mwa wanachama wake 164.
Waziri huyo wa zamani wa fedha na mambo ya kigeni wa Nigeria, ambaye alichukua usukani Machi 2021, anadhamiria kuifanya WTO kuwa mchangiaji muhimu katika jukwaa la kimataifa.
Okonjo-Iweala anatumai kufanikisha makubaliano yaliyotafutwa kwa muda mrefu ya kudhibiti ruzuku hatari za uvuvi. Mazungumzo ya kupiga marufuku ruzuku zinazohimiza uvuvi wa kupita kiasi na kutishia uendelevu wa hifadhi za Samaki yamekuwa yakiendelea katika WTO kwa zaidi ya miongo miwili. India jana ilisisitiza kuwa haitasaini makubaliano hayo bila ya kupewa msamaha wa kipindi cha miaka 25, muda ambao wengi hawakubaliano nao.
Kando na uvuvi, mkutano huo wa WTO unajaribu kufikia makubaliano kuhusu biashara ya mtandaoni, kilimo, upatikanaji wa chakula, hakimiliki za chanjo za Covid-19, namna WTO inavyoyashughulikia magonjwa ya mripuko, na mageuzi ya shirika hilo lenyewe.
Mawaziri wanajadili uwezekano wa kuweka msamaha wa muda kwa hakimiliki za chanjo za Covid-19. Hii ni kwa ajili ya kuzisaidia nchi zaidi kuanza kutengeneza chanjo hizo. Lakini kuna pingamizi kubwa kutoka kwa baadhi ya nchi ambazo zina makampuni makubwa ya dawa, kama vile Uingereza na Uswisi.
Pia hakujawa na makubaliano kuhusu kurefushwa kwa makubaliano ya kutoweka ushuru kwenye miamala ya kieletroniki. Nchi zilizostawi zinaunga mkono, wakati zinazoendelea zinapinga.
dpa, afpe