Mkuu wa idara ya ulinzi wa katiba Ujerumani ajiuzulu
3 Julai 2012Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Hans-Peter Friedrich, alieleza kuwa Bw. Fromm, mwenye umri wa miaka 63, ameamua kwa hiari yake kuachia madaraka. Fromm anatambulika kama mtaalamu wa masuala ya usalama mwenye ujuzi wa miaka mingi.
Jumatano iliyopita ilifahamika kwamba idara kuu ya ulinzi wa katiba Ujerumani aliyokuwa akiiongoza, iliteketeza mafaili yaliyokuwa na taarifa juu ya kundi la kinazi mamboleo linalofahamika kwa jina la NSU. Kundi hilo liliwaua watu tisa, raia wa Ujerumani wenye asili ya Uturuki na Ugiriki pamoja na polisi mmoja wa kike. Mauaji hayo yalifanyika katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi 2006.
Kiongozi wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, katika Bunge la Ujerumani, Wolfgang Bosbach, alieleza kuwa uchunguzi kuhusu kosa la kutetekeza mafaili utaendelea. "Tunataka kujua ni nani aliyeamuru mafaili yatetekezwe na kwa sababu gani. Nani alikuwa na taarifa kuhusu jambo hili? Upelelezi ukikamilika ndio tutakapojadili kuhusu hatua zaidi," alisema mwanasiasa huyo.
Upinzani wataka hatua zaidi zichukuliwe
Mbali na habari juu ya kuteteketzwa kwa mafaili yenye taarifa za upelelezi, hivi sasa imefahamika pia kuwa idara kuu ya ulinzi wa katiba, mwaka 2003 iliarifiwa juu ya kuwepo kwa mtandao wa makundi ya kigaidi yenye mtazamo wa kinazi mamboleo. Gazeti la hapa Ujerumani la Berliner Zeitung limeripoti kuwa waraka uliotumwa na idara ya ulinzi ya Italy, AISI, kwenda kwa idara kuu ya ulinzi wa katiba ya Ujerumani mwaka 2011, unaonyesha kuwa Italy iliionya Ujerumani kuhusu kukutana kwa wanazi mamboleo wa nchi mbali mbali za Ulaya katika mji wa Waasmunster, Ubelgiji, mwaka 2002. Waraka huo unaeleza pia kuwa upo uwezekano wa wanazi mamboleo kutoka Italy na Ujerumani kupanga mashambulizi ya kigaidi yanayowalenga watu wasio raia wa nchi za Ulaya.
Vyama vya upinzani katika bunge la Ujerumani havijaridhishwa na kujiuzulu kwa Fromm. Kwa mtazamo wao, Fromm ametolewa mhanga na hilo si jambo linalosaidia katika kufichua makosa yaliyofanyika katika idara kuu ya ulinzi wa katiba. Kiongozi wa chama cha walinda mazingira katika bunge, Renate Künast, amesema kuwa kuteketezwa kwa mafaili si kosa pekee lililotendeka katika idara ya ulinzi wa katiba na kuongeza kuwa idara hiyo sasa iko katika hali ya vurugu. Naye katibu mkuu wa chama cha Social Democratic Party SPD, Bi Andrea Nahles, amesema kuwa sasa ni wakati wa kutafakari kuhusu muundo wa taasisi za usalama za Ujerumani.
Mwandishi: Birkenstock, Günther
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Othman Miraji