1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa jeshi la Misri aitisha maandamano

Admin.WagnerD24 Julai 2013

Mkuu wa jeshi nchini Misri Jenerali Abdel Fattah al Sissi amewataka raia wa nchi hiyo kufanya maandamano makubwa kuliunga mkono jeshi na polisi katika kile alichokitaja kukabiliana na ghasia na ugaidi

https://p.dw.com/p/19DlP
Picha: Reuters

Huku hali  nchini humo ikiwa bado tete kufuatia kung'olewa madarakani na jeshi kwa Mursi mapema mwezi huu,mwito huo wa al Sisi unazua uwezekano wa machafuko zaidi nchini Misri kati ya wafuasi wa Mursi na wanaompinga.

Akihutubu katika sherehe za kufuzu kwa makadeti wa jeshi mjini Alexandria,al Sisi aliwahimiza wamisri kuandamana Ijumma hii akisema kujitokeza kwao kwa wingi kutampa mamlaka na agizo la kufanya lile linalohitajika kumaliza umwagikaji wa damu nchini humo.Mkuu huyo wa majeshi amewaahidi watakaojitokeza kuandamana kuwa watapewa ulinzi.

Tangu jeshi limpindue Mursi madarakani wiki tatu zilizopita,wafuasi wake wamekuwa wakiandamana wakiapa kuendelea na maandamano hadi arejeshwe madarakani.Makabiliano yamezuka mara kadhaa kati ya makundi pinzani huku kiasi ya watu 170 wakiuawa tangu mwishoni mwa mwezi uliopita wengi wakiwa ni wanaomuunga mkono Mursi.

Maandamano nchini Misri tangu kung'olewa madarakni kwa Mohammed Mursi
Maandamano nchini Misri tangu kung'olewa madarakni kwa Mohammed MursiPicha: Reuters

Kuanzia Jumatatu wiki hii watu 13 wamepoteza maisha yao nchini humo.Msemaji wa Rais  Ahmed  Al Muslimani amelaani ghasia hizo na kusema Misri si Syria ya pili na yeyote anayeilekeza huko ni msaliti.

Mashambulizi yaongezeka Sinai

Baada ya matamshi hayo ya mkuu wa jeshi hii leo,duru za kiusalama zimeripoti kuwa mwanajeshi mmoja ameuawa na watu waliokuwa na sialaha katika rasi ya Sinai ambako wanamgambo wamekuwa wakifanya mashambulizi kila siku tangu kuondolewa madarakani kwa Mursi.

Mripuko  ulitokea mbele ya kituo cha polisi cha Mansura katika jimbo la Nile Delta na mkuu wa huduma za dharura wa eneo hilo Mohammed Sultana amesema watu 28 wamejeruhiwa na mmoja amefariki.

Kiongozi mmoja wa udugu wa kiislamu Essam al Erian amesema wafuasi wa Mursi hawatatishwa na mwito huo wa al Sisi wa kufanyika maandamano.Erian amesema kupitia ukurasa wa facebook kuwa vitisho hivyo havitawazuia mamilioni ya watu kuendeleza maandamano.

Makabiliano kati ya wafuasi wa Mursi na wanaompinga yamzua hali ya taharuki
Makabiliano kati ya wafuasi wa Mursi na wanaompinga yamzua hali ya taharukiPicha: AFP/Getty Images

Hali ya taharuki yazidi Misri

Vuguvugu la Tamarod liliondaa maandamano makubwa yaliyopelekea kung'olewa madarakani kwa Mursi nalo limewataka wafuasi wake kumiminika mabarabarani Ijumma hii kuliunga mkono jeshi la nchi hiyo na kushurutisha kufunguliwa kwa mashitaka dhidi ya viongozi wa utawala uliong'olewa madarakani.

Kundi la udugu wa kiislamu leo limesusia kikao cha ufunguzi cha kongamano la maridhiano kinachodhaminiwa na Rais wa muda Adly Mansour.Kikao hicho kilisimamiwa na makamu wa rais wa muda Mohammed El Baradei.

Al Sisi amesema hana nia hata kwa sekunde moja kubatilisha msimamo wake kuhusu mchakato wa kisiasa aliotangaza siku aliyong'olewa madarakani Mursi inayojumuisha kuandaliwa chaguzi za Urais na bunge mapema mwaka ujao na kura ya maoni kuhusu katiba mpya kabla ya hapo au kufanyiwa marekebisho rasimu iliyoandikwa na washirika wa Mursi na kuahidi kuwa wachunguzi wa Umoja wa mataifa na wa umoja wa ulaya wataalikwa kufuatilia chaguzi hizo.

Mwandishi:Caro Robi/ap/Afp

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman