1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkuu wa WFP Mogadishu akamatwa na wanajeshi wa serikali

Saumu Mwasimba17 Oktoba 2007

Wanajeshi wa serikali ya mpito ya Somalia wamevamia ofisi za shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa WFP mjini Mogadishu na kumkamata mkuu wa shughuli za shirika hilo.

https://p.dw.com/p/C7hI
WFP limesimamisha shughuli za kutoa msaada Mogadishu
WFP limesimamisha shughuli za kutoa msaada MogadishuPicha: AP

Tukio hilo limefanyika saa chache baada ya wanajeshi wa Somalia kupambana vikali na wanamgambo katika mapigano ya usiku kucha ambapo watu wane waliuwawa.

Katika tukio hilo lililowashangaza wafanyikazi wa shirika hilo la Umoja wa mataifa,Idriss Osman mkuu wa shirika hilo katika Somalia alikamatwa na kupelekwa katika makao makuu ya usalama bila ya kujua chanzo cha kukamatwa kwake.

Katika taarifa yake shirika la umoja wa mataifa la Wfp limesema Serikali ya Somalia imekataa kutaja sababu za kumkamata afisa wake na kuongeza kwamba hatua iliyochukuliwa inakiuka sheria za kimataifa.

Kufuatia kisa hicho shirika la WFP limesimamisha shughuli zake zote katika mji mkuu wa Somalia.

Hakuna risasi zilizofyetuliwa wakati wa kisa hicho lakini inadaiwa kiasi cha wanajeshi 60 walikuja kwa malori wakiwa na bunduki walivamia eneo la afisi za shirika hilo na kumtia mbaroni bwana Osman.

Hata hivyo waziri wa mambo ya ndani Mohammed Mohamoud Guled amekanusha habari hizo lakini ameongeza kusema kwamba shirika la WFP mwezi uliopita liligawa chakula cha msaada bila ya kuishauri serikali jambo ambalo liliifanya serikali katika miezi ya hivi karibuni kuzuia shughuli za kugawa misaada katika sehemu ambazo zinawatu wanaoipinga serikali.

Msemaji wa WFP mjini Nairobi nchini Kenya Peter Smerdon amesema shirika hilo linaibebesha dhamana juu ya suala hilo serikali ya mpito.

Osman amekamatwa ikiwa siku mbili baada ya shirika hilo kuanza tena shughuli za ugawaji wa chakula cha msaada kwa watu 75,600 katika mji wa Mogadishu,shughuli ambayo ilikuwa imesimamishwa mwezi juni.

Itakumbukwa kwamba ghasia nchini Somalia zimeyalazimu mashirika mengi ya kutoa misaada ya kiutu kuondoka nchini humo na kuyaacha yale ya Umoja wa mataifa na machache mengine yanayotegemea wafanyikazi wa kisomali kuendesha shughuli kidogo zilizosalia.

Usiku kucha kumeripotiwa mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na wanamgambo ambapo watu wane waliuwawa na kiasi cha wengine 34 wakajeruhiwa.

Mapigano yanazidi kupamba moto kila uchao katika nchi hiyo ambayo imekuwa bila ya serikali madhubuti tangu mwaka 1991 alipongolewa madarakani Dikteta Siad Barre.

Mashambulio pamoja na mapigano kati ya koo zinazopingana yamesababisha mamia kwa maelfu ya wasomali kuukimbia mji mkuu Mogadishu.