Watu watatu wauawa kufuatia mlipuko wa gesi jijini Nairobi
2 Februari 2024Naibu Inspekta Mkuu wa polisi Douglas Kanja amesema kuwa watu 21 walitibiwa eneo la mkasa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Tukio hilo la usiku wa kuamkia leo, limeitumbukiza nchi ya Kenya katika majonzi na masikitiko makubwa. Kwa mujibu wa Polisi, mkasa huo ulisababishwa na Lori ambalo lilikuwa limebeba mitungi ya gesi, Iliyolipuka na kusababisha moto, moto huo uliteketeza mabohari yaliyokuwa karibu na hata makazi ya watu na kusababisha maafa.
Alfred Juma aliyeshuhudia mkasa huo amesema, "Leo saa tano usiku kuna mama aliniambia kuna gesi imelipuka, nikaamsha watu ili wasichomoke, nikaambia dereva wa lori asiwashe gari alipowasha gari lenyewe, mitungi ya gesi ikalipuka. Moto ukashika majengo."
Moto huo pia uliteketeza magari kadhaa na mali za biashara, ikiwa ni pamoja na majengo ya biashara nyingi. Kufuatia mkasa wenyewe Idara ya upelelezi imepewa saa 48 kuhitimisha uchunguzi.
Soma pia: Watano wafa baada ya ndege mbili kugongana na kuwaka moto Tokyo
Hata hivyo maswali yanazidi kuulizwa kuhusu mabohari ya gesi ambayo yamejengwa karibu na makazi ya watu.
Alfred Juma ameobgeza, "Kwa kweli hii kitu haistahili kungejengwa mahali wananchi wanaishi, sababu kama haingekuwa hapa hatungepata maafa ambayo tumepata."
Waathirika wengine wanatibiwa katika hospitali ya taifa ya Kenyatta
Baadhi ya waathirika 21 wanatibiwa katika hospitali ya Taifa ya Kenyatta, 160 katika Hospitali ya Mama Lucy, 19 katika Hospitali ya Mbagathi, 14 katika Hospitali ya Modern Komarock, na wanane katika Hospitali ya Nairobi West.
Daktari Martin Wafula ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa Hospitali ya Mama lucy amesema, "Ambulensi ambazo tumetumia usiku wa leo ni 15, ambulensi za Nairobi kaunti na zima moto, zingine tumerudisha kwa mahospitali kwa sasa tumebakisha saba, ikiwa kutatokea dharura."
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji wa serikali Isaac Mwaura amesema kuwa eneo la janga limehakikishiwa usalama, na kituo rasmi tayari kimeanzishwa kusaidia kuratibu operesheni za uokoaji na nafuu nyingine kwa wahanga.
Soma pia: Serikali ya Kenya kupinga uamuzi wa mahakama kuzuia polisi kwenda Haiti
Serikali imewaomba Wakenya kuondoka eneo lililofungwa ili kuruhusu shughuli za uokoaji kufanyika bila usumbufu mkubwa.
Hata hivyo moto huo ulidhibitiwa mapema Ijumaa asubuhi, lakini wazima moto, makundi ya uokoaji, na polisi walikuwa wakitafuta watu waliokwama eneo hilo. Kwa mujibu wa mamlaka huenda kiwango cha maafa kitaongezeka.
Serikali ya kaunti ya Nairobi imesema kuwa haitawatoza ada yoyote waliojeruhiwa kwenye mkasa huo ambao umeacha wingu jeusi katika taifa la Kenya.