1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaJapan

Mmoja apoteza maisha ajali ya helikopta za jeshi Japan

21 Aprili 2024

Mtu mmoja amefariki na wengine saba hawajulikani waliko leo baada ya ajali ya usiku wa kuamkia leo ambapo helikopta mbili za kijeshi za Japan zimegongana na kisha kuanguka baharini.

https://p.dw.com/p/4f1Gg
Mfano wa helikopta ya jeshi la Japan zilizopata ajali.
Mfano wa helikopta ya jeshi la Japan zilizopata ajali. Picha: Offizielle Website der Japanischen Maritimen Selbstverteidigungskräfte/AP Photo/picture alliance/dpa

Msemaji wa jeshi la ulinzi la Japan - SDF amethibitisha tukio hilo akisema mtu mmoja aliokolewa lakini baadae akathibitishwa kufariki.

Waziri wa Ulinzi Minoru Kihara amesema waokoaji walikiona kile kilichosadikika kuwa kipande cha helikopta hiyo baharini na wanaamini vyombo hivyo viwili viligongana.

Maafisa wanasema helikopta hizo huenda ziligongana na kuanguka wakati wa mafunzo ya usiku ya jinsi ya kukabiliana na mashambulizi ya nyambizi karibu na Visiwa vya Izu katika Bahari ya Pasifiki.

Vifaa vya kurekodi sauti za ndege hizo vilipatikana karibu na eneo la mabaki na vinafanyiwa uchunguzi, huku maafisa wakiwahoji marubani waliokuwa katika helikopta ya tatu ambayo ilikuwa inashiriki katika mazoezi hayo lakini haikuhusika katika ajali hiyo.