1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mnangagwa aahidi mageuzi Zimbabwe

24 Novemba 2017

Rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ameahidi kufanya mageuzi kadhaa nchini humo kuimarisha uchumi, uekezaji na demokrasia

https://p.dw.com/p/2oCqu
Simbabwe Harare Vereidigung Präsident Emmerson Mnangagwa
Picha: Reuters/M. Hutchings

Rais mpya wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa ambaye ameapishwa leo ameahidi kufanya mageuzi kadhaa katika kile kinachoonekana kutoa uhakikisho kwa wawekezaji wa kimataifa. Amesema amejitolea kupambana na umaskini na ufisadi. 

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, rais mpya wa Zimbabwe; Emmerson Mnangagwa; mwenye umri wa miaka 75, alitangaza mpango wake wa mabadiliko ambapo ameahidi kugeuza sera nyingi maarufu za mtangulizi wake Robert Mugabe aliyejiuzulu mapema wiki hii.

Amesema serikali yake itawafidia wakulima walowezi ambao ardhi zao zilichukuliwa na atawalinda wawekezaji wa kimataifa nchini humo, sambamba na kuanza mahusiano mapya na nchi za kigeni. Mnangagwa pia amesema uchaguzi ujao utafanyika jinsi ambavyo umeratibiwa kufanyikwa mwaka 2018.

Serikali ya Mnangagwa kukuza demokrasia

Emmerson Mnangagwa na mkewe Auxillia walipowasili katika uwanja wa sherehe za kuapishwa kwake mjini Harare
Emmerson Mnangagwa na mkewe Auxillia walipowasili katika uwanja wa sherehe za kuapishwa kwake mjini HararePicha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

"Serikali yangu itahakikisha mihimili ya demokrasia imeimarishwa na kuheshimiwa. Tuthibitisha kikamilifu uanachama wetu katika familia ya mataifa na tunajitolea kikamilifu kutekeleza wajibu wetu katika jumuiya zote za kikanda, bara na mashirika ya kimataifa ili kuchangia katika ukuaji wa dunia ya amani na maendeleo."

Maelfu kwa maelfu walihudhuria sherehe hiyo, pamoja na viongozi mbalimbali, miongoni mwao rais wa Zambia, Edgar Lungu, rais wa Botswana, Ian Khama, rais wa kwanza wa Zambia, mstaafu Kenneth Kaunda, na kiongozi wa upinzani wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai.

Uingereza, ambayo iliitawala Zimbabwe, ilimtuma waziri wake wa masuala ya Afrika kuiwakilisha, huku Jacob Zuma wa Afrika Kusini akituma udhuru kutohudhuria.

Mnangagwa: Mugabe astahili heshima na pongezi

Baada ya kula kiapo, Mnangagwa alikabidhiwa ala za uongozi ikiwemo mkufu maalum, huku wakuu wa vikosi vya usalama wakiapa kuwa watiifu kwake. Mnangagwa aliyewasihi Wazimbabwe kuyasahau maovu yaliyofanywa kale, na badala yake wafanye kazi kwa ushirikiano aliongeza kuwa licha ya kuondoka kwake alivyoondoka, Robert Mugabe ataendelea kupewa heshima ya hali ya juu. Mnangagwa ameongeza kuwa:

Emmerson Mnangwa pia anaitwa kwa jina la utani la 'Mamba'
Emmerson Mnangwa pia anaitwa kwa jina la utani la 'Mamba'Picha: Getty Images/AFP/M. Longari

"Komredi Robert Gabriel Mugabe, alituongoza katika ukombozi wa taifa, alichukua majukumu ya uongozi wakati wa changamoto tele, kwa manufaa ya nchi yetu. Hilo linastahili pongezi na kusherehekewa siku zote. Tukubali tutambue wajibu wake mkubwa wa kutumikia nchi yetu."

Wakosoaji waonya kumhusu Mnangagwa

Mnangagwa amechukua urais baada ya utawala wa kiimla wa Mugabe ambao ulidumu kwa miaka 37.

Hata hivyo, wakosoaji wameonya kuwa Mnangagwa, ambaye ukatili wake ulimpa jina la utani la 'Mamba' na ambaye amelaumiwa kwa kusimamia machafuko na mauaji ya kikabila, huenda akawa na utawala wa kiimla kama mtangulizi wake.

Hadi alipojiuzulu, Mugabe ndiye alikuwa rais mwenye umri mkubwa zaidi akiwa wa miaka 93.

Zimbabwe ambayo iliwahi kuwa na uchumi wenye matumaini, imeporomoka chini ya utawala wa Mugabe. Ukosefu wa ajira nchini humo unakadiriwa kuwa wa asilimia 90. Wazimbabwe wengi wameelezea furaha na matumaini makubwa kwamba Mnangagwa ataleta mageuzi na uekezaji zaidi.

Mwandishi: John Juma/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef