1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mnangagwa mshindi urais Zimbabwe

Isaac Gamba
3 Agosti 2018

Tume ya uchaguzi  Zimbabwe imemtangaza Emmerson Mnangagwa wa chama tawala  ZANU-PF mshindi wa kinyan'ganyiro cha  urais katika  uchaguzi  uliofanyika Jumatatu.

https://p.dw.com/p/32ZJ2
Simbabwe Wahl | Emmerson Mnangagwa, Präsident
Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

 Kwa mujibu wa matokeo hayo Mnangagwa, mshirika wazamani wa Robert Mugabe ameshinda baada ya kujipatia asilimia 50.8 ya kura dhidi ya Nelson Chamisa wa chama cha upinzani  MDC aliyepata asilimia 44.3 ya kura na hivyo tume ya uchaguzi kumtangaza rasmi Mnangagwa mshindi wa nafasi ya urais.

Akitangaza matokeo hayo  jimbo kwa jimbo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi  Priscila Chigumba alisema Kura alizopata mgombea wa chama cha ZANU-PF Emerson Mnangagwa ni zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa za nafasi ya urais hivyo anamtangaza rasmi Mnangagwa Emerson Ndabudzo wa chama cha ZANU-PF kuwa mshindi na rais mteule wa Zimbabwe kuanzia leo tarehe 3 August 2018.

Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wa Twitter Mnangagwa aliwashukuru  Wazimbabwe kwa kumchagua kushika nafasi hiyo na kusema ingawa wanaweza kuwa wamegawanyika kutokana na kura zilizopigwa lakini  huu sasa  ni mwanzo mpya.

 Ili kutangazwa mshindi wa nafasi ya urais mgombea anatakiwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Mgombea wa chama cha upinzani MDC alifanya vizuri katika maeneo ya mjini wakati Mnangagwa alipata kura nyingi vijijini.

Uchaguzi huo umefanyika kujaribu kurejesha demokrasia nchini humo kufuatia miaka 37 ya utawala wa ukandamizaji chini ya kiongozi wa muda mrefu Robert Mugabe.

 

Upinzani wayakataa  matokeo

Nelson Chamisa
Mgombea wa chama cha MDC- Nelson ChamisaPicha: DW/P. Musvanhiri

Chama cha upinzani MDC kimesema kitayapinga matokeo hayo mahakamani na kuongeza kuwa kilichopelekea tume ya uchaguzi kuchelewa kutangaza matokeo ilikuwa ni kufanya wanachotaka kuhusiana na matokeo hayo.

 Ama kwa upande wake mgombea wa upinzani Nelson Chamisa amesema polisi  walivamia makao makuu ya chama hicho na kuzuia kompyuta huku waranti ya kufanya upekuzi ikionesha walikuwa wakitafuta silaha zisizo sajiliwa. Watu 16 walitiwa mbaroni kufuatia tukio hilo.

Hayo yanajiri huku rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akitoa mwito hii leo  kwa wazimbabwe kukubali kuchaguliwa kwa Mnangagwa kuwa rais wa nchi hiyo na iwapo wana pingamizi lolote wafuate taratibu za kisheria.

Tangu Zimbabwe ijipatie uhuru kutoka  kwa Waingereza mwaka 1980 taifa hilo limekuwa na marais wawili tu ikiwa ni pamoja na Mugabe aliyeongoza kwa mkono wa chuma katika kipindi cha miaka 37 na mshirika wake wa zamani Emerson Mnangagwa aliyeteuliwa kushika madaraka hayo baada ya Mugabe kujiuzulu Novemba mwaka jana kufuatia shinikizo la jeshi.

Watu sita waliuawa Jumatano iliyopita wakati wanajeshi walipofyatua risasi dhidi ya waandamanaji wa chama cha upinzani waliokuwa  wakidai kuna udanganyifu katika uchaguzi huo.

Wanajeshi  pamoja na polisi waliweka ulinzi mkali mjini Harare wakiwaaamuru watembea kwa miguu na wafanyabiashara kuondoka maeneo hayo huku chama cha upinzani cha MDC kikisisitiza kuwa chama tawala ZANU-PF kilikuwa kikijaribu kufanya udanganyifu.

Idadi ya wapiga kura waliojitokeza kushiriki uchaguzi ilikuwa ni asilimia 80 karibu katika majimbo yote kumi ya nchi hiyo.

Chama tawala ZANU-PF pia kinaripotiwa  kushinda kirahisi katika uchaguzi wa bunge uliofanyika Jumatatu.

Kabla ya vurugu za baada ya uchaguzi waangalizi wa Umoja wa Ulaya walisema  hakukuwa na mazingira sawa kwa vyama vyote wakati wa mchakato wa uchaguzi huo huku waangalizi wa Umoja wa Ulaya  katika taarifa yao waliyoitoa baada ya vurugu za Jumatano walilaani matumizi ya nguvu dhidi ya raia wasio na silaha.

Kiongozi wazamani wa Zimbabwe Robert Mugabe ambaye awali aliwataka  wapiga kura kukitaa chama tawala ZANU-PF alipiga kura Jumatatu   pamoja na mkewe mjini Harare.

 Rais mteule Mnangagwa sasa atalazimika  kufufua uchumi wa taifa hilo ulioporoka wakati wa Mugabe na kutafuta suluhisho la ukosefu wa ajira ikiwa ni pamoja na kukabiliana na mfumuko wa bei.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE/RTRE/DW

Mhariri: Iddi Ssessanga