Mnangagwa: Yaliyofanywa na vikosi vya usalama hayakubaliki
22 Januari 2019Rais Mnangagwa ambaye amerejea nchini humo Jumatatu jioni baada ya kusitisha safari yake kuelekea Jukwaa la Kiuchumi Duniani mjini Davos, Uswisi, aliandika katika ukurasa wa Twitter kwamba "vitendo vya vurugu na utovu wa nidhamu vilivyofanywa na vikosi vya usalama havikubaliki na vinaisaliti Zimbabwe mpya".
Lakini pia alikosoa vikali maandamano yaliyogubikwa na fujo na uporaji, akieleza kwamba "kila mmoja ana haki ya kuandamana, lakini hayo kilichoshuhudiwa wiki iliyopia hakikuwa maandamano ya amani." Maandamano hayo yalitawaliwa na vurugu, uharibifu wa kijinga, uporaji wa vituo vya polisi, wizi wa silaha na sare, uchochezi na vitisho vya vurugu, kwa mujibu wa rais Mnangagwa. Ametoa wito wa kufanyika "mjadala wa kitaifa" miongoni mwa vyama vya kisiasa.
Alitoa kauli hizo alipowasili mjini Harare Jumatatu jioni baada ya kukatisha ziara yake kimataifa iliyokuwa ikitafuta uwekezaji. Maandamano ya wiki iliyopita yaliyochochewa na uamuzi wa serikali wa kuongeza bei ya mafuta, yalikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa jeshi na polisi.
Watu wapatao 12 waliuawa na wengine 78 wanapatiwa matibabu kutokana na majereha ya risasi, kwa mujibu wa asasi ya haki za binadamu ya Zimbabwe, ambayo iliorodhesha matukio zaidi ya 240 ya kushambuliwa na mateso.
Jeshi la nchi hiyo lilionekana mitaani wiki iliyopita kwa mara ya kwanza tangu vurugu za baada ya uchaguzi mwezi Agosti ambapo watu sita waliuawa. Wakati huu, inasemekana kulikuwa na msako wa watu majumbani uliotekelezwa na vikosi vya usalama.
Mnangagwa alikiambia kituo cha taifa cha utangazaji kuwa ziara yake nchini Urusi na Kazakhstan ilikuwa ya manufaa sana na itainufaisha Zimbabwe siku za usoni. Wakati wa ziara yake alikutana na rais wa Urusi Vladmir Putin na kuomba mkopo.
Polisi walimkamata katibu mkuu wa Baraza la vyama vya wafanyakazi Japhet Moyo na kumshitaki kwa kuratibu mgomo wa nchi nzima wa wiki iliyopita. Serikali pia ilifunga huduma ya intaneti nchi nzima lakini mahakama ya juu iliamuru serikali kurejesha huduma hiyo ikisema waziri wa ulinzi hakuwa na mamlaka ya kutoa amri hiyo bali ni rais pekee.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AP/AFP
Mhariri: Josephat Charo