Mnangagwa:Ni enzi mpya ya demokrasia kamili Zimbabwe
23 Novemba 2017
Akiwahutubia mamia ya wafuasi wake katika makao makuu ya chama tawala nchini humo, ZANU-PF usiku wa Jumatano muda mfupi baada ya kurudi nchini, Emmerson Mnangagwa alisema ''leo tunashuhudia mwanzo mpya wa demokrasia kamili nchini mwetu.''
Ilikuwa kauli yake ya kwanza hadharani tangu tarehe sita Novemba, siku aliyofukuzwa na Robert Mugabe kutoka wadhifa wa Makamu wa Rais, katika mvutano wa kuwania nafasi ya kurithi madaraka ya urais, kati yake (Mnangagwa) na mke wa rais, Grace Mugabe.
Ni mvutano huo na mgogoro uliofuata, ambao ulilifanya jeshi kuingilia kati, na kuanzisha mchakato uliomlazimisha Rais Mugabe kusalimu amri na kuachia madaraka, baada ya kuzidiwa na shinikizo kutoka chama chake mwenye.
Arejea na heshima ya urais
Tangu wakati huo alikuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini, na hapo jana alisafirishwa kwa ndege kurudi nyumbani, na kutua katika uwanja wa Manyame alikopokelewa na vigogo wa chama tawala, na kusafiri katika msafara wa magari mithili ya ule wa rais hadi Ikulu.
Katika hotuba yake kwenye makao makuu ya ZANU-PF ambayo ilirushwa moja kwa moja kwa njia ya televisheni, Mnangagwa alisisitiza umoja na haja ya kuufufua uchumi.
''Hakuna aliye muhimu kuliko mwingine, wote tuko wazimbabwe,'' amesema kiongozi huyo na kuongeza, ''tunataka kuukuza uchumi wetu, tunataka amani katika nchi yetu, na fursa za kazi, kazi, nchini mwetu...''
Hotuba hiyo ya Emmerson Mnangagwa ambaye si mgeni katika siasa za Zimbabwe ilipokelewa kwa hisia tofauti. Kwa vijana wasio na ajira kama Remigio Mutero ambaye ni mhitimu wa chuo kikuu katika teknolojia ya komputa, hotuba hiyo ilikuna pale panapowasha.
''Ilikuwa hotuba nzuri kabisa, tunachotaka ni fursa za ajira'', alisema Mutaro baada ya kumsikiliza Mnangagwa.
Lakini Edgar Mapuranga, mwajiriwa katika sekta ya ulinzi wa mali binafsi, alisema haoni tofauti kati ya Mnangagwa na mtangulizi wake.
''Robert Mugabe ameondoka, lakini sioni Mnangagwa akifanya chochote tofauti na mkongwe huyo. Haya sio mabadiliko niliyoyatarajia, lakini ngoja tumpe muda'', alisema Mapuranga.
Watakaonufaika ni wale wale
Mjumbe maalumu wa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani barani Afrika, Guenther Nooke, amesema ingawa Mnangagwa anatarajiwa kushinda katika uchaguzi ujao bila taabu, huo utakuwa ushindi wa kundi lile lile lililokuwa na ushawishi chini ya Mugabe, kwa kusaidiwa na China.
''Atapata ushindi kwa kutumia hila na vitisho, na kisha, tutashuhudia madaraka yakihama kutoka kiongozi mmoja wa kiimla, na kuangukia mikononi mwa mwingine wa aina hiyo'', amesema mjumbe huyo wa Kansela Merkel.
Mnangagwa ambaye amekuwa mshirika wa karibu wa Robert Mugabe tangu enzi za kupigania uhuru, anaandamwa na tuhuma za kuhusika katika visa vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu vilivyofanywa na serikali ya Robert Mugabe, vikiwemo uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi, na ukandamizaji wenye umwagaji mkubwa wa damu dhidi ya vuguvugu la upinzani wa watu wa kabila la Ndebele. Binafsi anatajwa kuwa mtu mwenye msimamo mkali na asiye na huruma.
Mshauri mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kushughulikia Mizozo - ICG Kusini mwa bara la Afrika Piers Pigou, amesema doa hilo la siku za nyuma halitafutika katika mustakabali wa Mnangagwa. ''Litamfuata kokote aendako kama pande la Chingamu lililonasa katika unyayo wa kiatu chake'', amesema Pigou.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre
Mhariri: Ommilkheir Hamidou