1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mo Farah ashindwa kung'ara katika marathon

14 Aprili 2014

Alijiunga na magwiji wenzake kwa mazoezi ya wiki mbili katika maeneo ya nyanda za juu nchini Kenya, na wengi walisubiri kuona kama angeupita mtihani wa kukimbia mbio za marathon kwa mara ya kwanza maishani mwake.

https://p.dw.com/p/1Bhnr
Leichtathletik WM Moskau Mo Farah
Picha: Reuters

Na baada ya mbio kumalizika, Mo Farah, hakuwa miongoni mwa wanariadha waliomaliza katika nafasi ya kwanza. Muingereza Mo Farah ambaye baada ya kumaliza mbio hizo katika nafasi ya nane, alisema bado yupo na atarejea barabarani mara nyingine kwa kishindo. Farah alisema "Bila shaka nitarudi tena, nina uhakika asilimia mia moja. Kwangu nilitaka kujaribu, London ni mji wangu, hapa ndio nilikulia, hivyo, na nilitaka kuwapa mashabiki wangu. Kivyangu nimesikitika kwamba sikushinda..ingekuwa vizuri niwafurahishe mashabiki lakini bila shaka nitarejea na kufanya vyema"

Bingwa anayeshikilia rekodi ya ulimwengu Mkenya Wilson Kipsang alishinda mbio za London Marathon kwa upande wa wanaume, wakati akiweka muda bora zaidi wa mbio hizo, saa mbili, dakika nne na sekunde 29.

Mbio za London Marathon huwavutia wanariadha mahiri kote ulimwenguni kila mwaka
Mbio za London Marathon huwavutia wanariadha mahiri kote ulimwenguni kila mwakaPicha: picture alliance/empics

Kipsang aliivunja rekodi ya awali ya muda bora wa mbio hizo za London iliyowekwa na Mkenya Emmanuel Mutai mwaka 2011 ya saa mbili dakika nne na sekunde 40. Ulikuwa ushindi wa pili wa London marathon kwake Kipsang, ambaye pia alishinda mwaka wa 2012, na mara hii alimzidi nguvu mkenya mwenyake Stanely Biwott kwa kumaliza wa kwanza. Muethiopia Tsegaye Kebede ambaye alishinda mwaka jana, alimaliza katika nafasi ya tatu wakati muethiopia mwingine Ayele Abshero akiridhika na nafasi ya nne.

Kenya ilisheherekea ushindi mara mbili wakati Edna Kiplagat aliyemaliza katika nafasi ya pili miaka miwili iliyopita, aliposhinda mbio za wanawake. Edna Kiplagat, ambaye pia ni bingwa mara mbili wa ulimwngu, alitumia muda wa saa mbili dakika 20 na sekunde 21 na kumpiku mkenya mwenzake Florence Kiplagat aliyefika jukwaani katika nafasi ya pili. Muethiopia Tirunesh Dibaba ambaye ni bingwa wa Olimpiki na ulimwengu katika mbio za mita 10,000 alimaliza katika nafasi ya tatu, kwenye mbio hizo za marathon alizoshiriki kwa mara ya kwanza katika maisha yake.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdulrahman