1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Modi ahofia vikwazo vya biashara huru

23 Januari 2018

Waziri mkuu wa India Narendra Modi ameelezea hofu yake dhidi ya kuongezeka kwa ulinzi wa biashara, vikwazo vya biashara huru miongoni mwa mataifa na kukosekana kwa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/2rN3E
Schweiz Davos - Indiens Premierminister Narendra Modi beim World Economics Forum (WEF)
Picha: Reuters/D. Balibouse

Waziri mkuu wa India Narendra Modi amesema hii leo kwamba kuongezeka kwa ulinzi wa biashara, ongezeko la vikwazo vya biashara huru miongoni mwa mataifa na kukosekana kwa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kunaashirikia kuibuka kwa kitisho kikubwa zaidi duniani katika nyakati za sasa. Modi amesema hayo katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano la uchumi duniani, WEF mjini Davos Uswisi. 

"Kinachoendelea hivi sasa ni kama vile kinakwenda kinyume na utandawazi" alisema Modi kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano la mwaka la WEF linalokutanisha washiriki 3,000 kutoka kada tofauti, kuanzia wanasiasa, maafisa, viongozi kutoka Umoja wa Mataifa, wasomi hadi wanaharakati wa kijamii. Modi ni waziri mkuu wa kwanza wa India kutoa hotuba ya ufunguzi wa kongamano hili.

Kuimarishwa kwa ulinzi wa masoko kunaongezeka kwa kasi alisema Modi, akiangazia ushuru mpya ambao ni kizingiti katika hatua za kuimarisha makubaliano ya biashara ya kimataifa pamoja na kudidimizwa kwa uwekezaji, hatua inayomsukuma kutoa mwito wa kushirikiana ili kukabiliana na kitisho hiki.

Matamshi haya ya Modi yanakinzana wazi na sera za rais wa Marekani Donald Trump, anayehamasisha sera yake ya "Marekani kwanza", hasa linapokuja suala la biashara. Trump anatarajiwa kuhutubia kongamano hilo siku ya Ijumaa, huku jana, Jumatatu serikali yake ikitangaza kupandisha kodi ya uingizwaji wa mashine kubwa za kufulia na bidhaa za umeme unaotumia nguvu ya jua, ikiwa ni hatua ya kuwalinda wazalishaji wake wa ndani.

Schweiz Davos Logo Weltwirtschaftsforum
Kongamano hilo litahitimishwa siku ya Ijumaa, ambapo Rais Donald Trump atahutubia Picha: picture-alliance/Photoshot/Xu Jinquan

Kiongozi wa kundi la wafanyabiashara kutoka Ujerumani ameonya kuhusu hatua hiyo ya rais Trump ya kupandisha kodi ya bidhaa hizo zinazoingizwa nchini Marekani kuwa utaleta matokeo ambayo hayakutarajiwa.

Hotuba hii ya Modi inaendana na baadhi ya vipengele vilivyozungumzwa na rais wa China, Xi Jinping katika hotuba yake aliyotoa kwenye kongamano kama hili mwaka jana. Jinping alipozungumza siku kadhaa kabla ya kuapishwa rais Donald Trump, aligusia nafasi ya China kama kiungo muhimu cha uchumi, akiahidi kuongeza uwazi katika suala la utandawazi. 

Kuhusu suala la mazingira, Modi alinukuliwa akisema mabadiliko ya tabianchi ni kitisho kingine kikubwa duniani, na bado dunia imeshindwa kuungana pamoja kukabiliana nayo. Wakati kila mmoja akizungumzia namna ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafu, ni mataifa machache sana yameonyesha kuunga mkono hatua hiyo kwa kuyasaidia mataifa masikini kama India, kwa rasilimali katika kufikia matumizi ya teknolojia mpya na rafiki kwa mazingira. 

Modi ameongozana na ujumbe mkubwa wa maafisa wa serikali na wafanyabiashara kwenye kongamano hilo la Davos, na ni waziri mkuu wa kwanza wa India kufanya hivyo katika kipindi cha miaka 21, akilenga kuitangaza India kama taifa linalokua kwa kasi zaidi kiuchumi na kiungo muhimu cha ukuaji wa dunia. Amesema serikali yake imejizatiti katika kuimarisha uchumi na kupunguza urasimu wa kufanya biashara na India, pamoja na kuvutia uwekezaji.

Mkurugenzi wa shirika la fedha, IMF Christine Lagarde, rais wa Rwanda Paul Kagame, rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa na makamu wa rais wa zamani wa Marekani, Al Gore ni miongoni wa waliohudhuria ufunguzi huo.

Mwandishi: Lilian Mtono./EAP/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman