Modi asifu uamuzi uliochukuliwa na India
15 Agosti 2019Magazeti nchini Pakistan yamechapisha matoleo yenye mipaka myeusi na wanasiasa akiwemo Waziri Mkuu Imran Khan wameziondoa picha zao kwenye mitandao ya kijamii na badala yake kuweka miraba myeusi.
Maandamano yanatarajiwa kufanyika kote nchini humo ikiwemo eneo la Azad Kashmir lililoko magharibi mwa eneo ambalo Pakistan inalitawala. Hatua hiyo ya kiishara inakuja wakati Wapakistan wakiwa wamevunjwa moyo kutokana na kukaa kimya kwa jamii ya kimataifa kuhusiana na mzozo huo wa Kashmir.
Uamuzi ulikuwa mojawapo ya hatua kubwa zaidi kwa utawala wa India
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ameitetea hatua yake ya kuiondolea Kashmiruwezo wa kujitawala wakati ambapo Khan ameonya kuhusiana na kutokea kwa mauaji ya kidini.
Katika hotuba yake ya kuadhimisha siku ya Uhuru wa India, Modi amesema uamuzi huo ulikuwa mojawapo ya hatua kubwa zaidi kuchukuliwa na utawala wake. Amesema fikra mpya zinahitajika baada ya miongo saba ya kufeli kuleta amani katika eneo hilo la Kashmir ambapo makumi kwa maelfu ya watu wamefariki katika miaka 30 iliyopita.
"Nina imani kamili kwamba chini ya muundo huu mpya, sote tutakuja pamoja na tuangamize ugaidi na ubaguzi Kashmir na Jammu," alisema Modi.
Urusi inasema inaunga mkono msimamo wa India katika mzozo huo
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lenye wanachama 15 huenda likaujadili mzozo huo Alhamis ingawa Pakistan inasema ina uhakika wa kuungwa mkono na China pekee ambayo inamiliki sehemu za Jammu na Kashmir.
Hapo Jumatano, Urusi ambayo ni mwanachama wa kudumu katika Baraza hilo la Usalama ilisema inaunga mkono msimamo wa India kwamba mzozo huo unastahili kusulishwa kwa mazungumzo ya nchi mbili, huku Marekani ikisema uamuzi wa India ni suala la ndani la nchi hiyo.
Kashmir imegawanywa kati ya India na Pakistan tangu ipate uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1947 na imekuwa chanzo cha vita viwili vikubwa na machafuko mengi kati ya nchi hizo mbili zenye silaha za nyuklia. Machafuko ya hivi majuzi yalishuhudia India na Pakistan zikirushiana makombora mnamo mwezi Februari.