Mohammed al-Bashir kiongozi wa mpito Syria
10 Desemba 2024Hatua hiyo inatekelezwa katika kipindi ambacho serikali ya Israel ikikanusha wanajeshi wake kufanya mashambulizi katika eneo lisilokuwa na shughuli za kivita la Syria.
Uamuzi wa Bashir unafuatia kuondolewa madarakani kwa rais Bashar al-Assad. Awali Jumatatu, vyombo vya habari vya mataifa ya Kiarabu viliripoti kwamba al-Bashir alikuwa amepewa jukumu la kuunda serikali mpya ya Syria baada ya mkutano wa viongozi wake wakuu.
Mkutano mwingine muhimu ulifanyika leo katika hoteli moja mjini Damascus, uliongozwa na kiongozwa na mkuu wa muungano wa waasi, Ahmed al-Sharaa aliefahamika pia kwa jina Abu Mohammed al-Joulani ulijumuisha mawaziri wa serikali iliyopita.
Uongozi wa mpito utadumu hadi Machi
Katika hotuba fupi kwenye televisheni ya serikali, Mohammed Bashir, mtu ambaye hajulikani sana katika sehemu kubwa ya Syria amesema ataongoza mamlaka ya muda hadi Machi Mosi.
Nyuma yake kulikuwa na bendera mbili. Kijani, nyeusi na nyeupe iliyopeperushwa na wapinzani wa Assad katika muda wote wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, na bendera nyeupe ya kiapo cha imani ya Kiislamu katika maandishi nyeusi, ambayo kwa kawaida hutumiwa huko Syria na wapiganaji wa Kiislamu wa madhehenu ya Sunni.
Recep Erdogan ambae ni Rais wa Uturuki ameipongeza hatua hiyo,"Kuanzia sasa, hatuwezi kuruhusu Syria igawanywe tena. hatuwezi kamwe kuruhusu eneo la nchi kuwa uwanja wa vita tena. Shambulio lolote dhidi ya uhuru wa watu wa Syria, uthabiti wa serikali mpya ya Syria, na uadilifu wa eneo la kale la Syria tutalishughulikia pamoja na watu wa Syria." Alisema kiongozi huyo wa Uturuki.
Kurejea kwa hali ya kawaida Damascus
Katika mji mkuu wa Syria, benki zilifunguliwa kwa mara ya kwanza tangu kupinduliwa kwa Assad. Maduka pia yalikuwa yakifunguliwa tena, idadi kubwa ya magari lirejea barabarani, mafundi ujenzi waliendelea na shughuli zao za marekebisho na ukarabati katikati mwa jiji la Damascus pamoja na wasafisha mitaa waliingia kazini.
Kunaelezwa pia kupungua kwa idadi ya watu wenye silaha mitaani. Vyanzo viwili vilivyo karibu na waasi vilisema kulitolewa amri ya wapiganaji kuondoka mijini na polisi kwa ajili ya usalama wa ndani wa kawaida kutoka katika kundi kuu la waasi, Hayat Tahrir al-Shams (HTS) wakapelekwa katika maeneo hayo.
Hatua ya kurejesha hali ya kawaida inatekelezwa licha ya kuwepo kwa hali mbaya ya mashambulizi ya anga kutoka Israel, yakilenga kambi za kijeshi za jeshi la Syria, ambalo vikosi vyake vimetoweka kutokana na nguvu ya kusonga mbele kwa wapiganaji waliomuondoa Assad.
Soma zaidi:Israel yafanya mashambulizi makubwa nchini Syria
Israel, ambayo imeripotiwa kutuma vikosi kuvuka mpaka katika eneo la Syria imesema mashambulizi yake ya anga yalilenga katika kuzuia silaha zisiangukie kwenye mikono yenye uadui. Na imekanusha ripoti kuwa vikosi vyake vilikuwa vimesonga mbele zaidi ya eneo lisilokuwa na shughuli za kijeshi la Syria na kufanya mashambani kusini magharibi mwa Damascus.