Mpango tata wa kutoa chango kwa mifugo Kenya kuanza Januari
19 Desemba 2024Hata hivyo, mjadala kuhusu utekelezaji wa zoezi hilo umeibua hisia kali, huku baadhi ya madaktari wa mifugo na wafugaji wakipendekeza usitishwe, kutokana na wasiwasi kuhusu uingiliaji wa wanasiasa, ulioathiri imani ya wananchi kwa zoezi hilo.
Waziri wa Kilimo na Mifugo nchini Kenya, Dakta Andrew Karanja, ametangaza kuwa mpango wa kuwachanja mifugo utazinduliwa kama ilivyopangwa mapema mwaka ujao, na kusema wanataka mifugo wote nchini humo kuchanjwa kwa wakati mmoja ili kukabiliana na magonjwa. "Tunataka kuratibu mipangilio pamoja na kaunti ili tunapoenda katika eneo moja kaunti zote zinapewa chanjo kwa wakati mmoja. Hii italipa zoezi lenyewe ufanisi zaidi."
Soma pia: Kenya yatangaza mpango wa kuanza kuwafidia wafugaji
Madaktari wa mifugo wanapendekeza kusitishwa kwa muda kwa zoezi la chanjo ili kutoa nafasi ya kushirikishwa kwa wadau wote. Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Muungano wa Madaktari wa Mifugo nchini (KVA) umesema kuwa hatua ya wanasiasa kuingilia mchakato huo imepunguza imani ya Wakenya kwa mpango huo.
Madaktari hao wanashauri serikali kuzingatia kukabiliana na magonjwa maalum katika maeneo yenye changamoto hizo badala ya kufanya chanjo ya pamoja ya ugonjwa mmoja katika maeneo ambako ugonjwa huo sio tatizo kubwa. Pia, wamesisitiza umuhimu wa kutoa muda zaidi kwa uhamasishaji wa umma kuhusu mpango huo na masuala yanayowatia wasiwasi.
Soma pia: Ukame wasababisha wafugaji Marsabit kupata hasara ya mamilioni
Taarifa hiyo inataka wadau wote wakiwemo madaktari wa mifugo wenye utaalamu, wakulima, na viongozi wa jamii kushirikishwa kikamilifu. Wamehimiza serikali kutoa taarifa za wazi kwa wananchi kuhusu chanjo hiyo na kuruhusu wakulima kufanya maamuzi huru kuhusu iwapo wanataka chanjo hiyo au la.
Madaktari wa mifugo pia wameitaka serikali kuepuka kutumia lugha kali au ya kulazimisha katika kuhamasisha umma kukubali chanjo hiyo. Aidha, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amemkosoa Rais William Ruto kwa kile alichokitaja kuwa matumizi ya lugha isiyofaa kwa wananchi kuhusu chanjo ya mifugo.
Akihutubia mnada wa kila mwaka wa mbuzi katika eneo la Kimanale, Kaunti ya Baringo, Rais William Ruto alisisitiza kuwa mpango wa chanjo ya mifugo utaendelea licha ya ukosoaji unaoendelea. Rais Ruto aliwataka wale wanaopinga mpango huo kuepuka kuingiza siasa katika mradi huo, akiwatuhumu kwa kueneza uvumi, taarifa potofu, na propaganda zisizo na msingi. "Ikiwa sio hatari kuwachanja wanadamu ni namna gani ni hatari kuwachanja wanyama? Eti tukiwachanja ng'ombe watakosa kunyamba, kwani sote tuliochanjwa tumekosa kunyamba?"
Baadhi ya viongozi kutoka maeneo ya ufugaji wanaoliunga mkono zoezi wamewarai wafugaji kuunga mkono chanjo kwa mifugo kwani itaboresha afya na soko la mifugo. Gavana wa Marsabit Mahamud Ali ametangaza kuanza kampeini ya kuwashawishi watu zaidi kukumbatia zoezi hilo.
Muungano wa madaktari wa mifugo unahimiza uwazi juu ya magonjwa yanayolengwa, ikiwa ni pamoja na sababu za chanjo, mizunguko mingapi ya chanjo itatekelezwa, na utambulisho wa wafadhili wa mpango huo wa chanjo.