Ureno yaboresha mpango wa viza ya dhahabu kuongeza mapato
10 Januari 2024Mpango huo, ambao unawapa matajiri wasio raia wa Umoja wa Ulaya wanaowekeza nchini Ureno haki ya kuishi nchini humo, umeingiza euro bilioni 7.3 tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2012, ambapo washiriki wengi wanatoka China, Brazil na Marekani. Takribani asilimia 90 ya fedha hizo ziliingia kwenye mali zisizohamishika, na hivyo kuibua malalamiko kuwa ilikuwa ikipandisha bei za nyumba katika moja ya mataifa maskini zaidi ya Ulaya.
Wakati huo huo, Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ilitoa wito wa kukomesha programu kama hizo, ikitaja hatari za kiusalama. Kuweka pesa katika mifuko ya uwekezaji lilikuwa chaguo chini ya mpango wa Ureno tangu mwaka 2015, lakini sasa inatarajiwa kuwa njia yake kuu. Njia nyingine ni pamoja na kuchangia miradi ya kitamaduni au utafiti.
Soma pia: EU, Ujerumani zataka Poland kujieleza kuhusu rushwa ya visa
Wakili Vanessa Lima, kutoka kampuni ya Prime Legal, ambayo inasaidi wageni kuomba viza miongozi mwa huduma nyingine, anasema biashara ya nyumba mara zote imeondoa nadhari kutoka machaguo mengine, na kuongeza kuwa aina kuu ya uwekezaji kuanzia sasa itakuwa katika wakfu. Ili kustahiki, waombaji lazima wahamishe kiasi cha euro 500,000 kwa mfumo mmoja au zaidi inayostahiki.
Mamlaka ya udhibiti wa soko la hisa la Ureno CMVM, ambayo inaidhinisha mifuko, ilisema haiwezi kutoa orodha ya mifuko itakayoshiriki katika mpango wa uwekezaji wa visa ya dhahabu, lakini Lima anakadiria kuwa kulikuwa na takriban mifuko 40, ingawa mingine inaweza bado kuwa tayari kwa uwekezaji.
Miongoni mwa mifuko inayotazamiwa kunufaika ni ule wa kilimo endelevu wa Pela Terra, ambao tayari unasaidia kufufua karibu hekta 1,000 za mashamba katika eneo la Alentejo.
Athari za kuondoa ununuzi wa nyumba
Ingawa hakuna data rasmi bado, wanasheria watatu waliobobea katika mpango wa viza ya dhahabu waliliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanatarajia mifuko hivi karibuni kuwakilisha asilimia 80-90 ya uwekezaji wote kama huo. Lakini kwa kuwa ununuzi wa nyumba umefungwa, wengine wanasema Ureno huenda ikaingiza fedha kidogo kwa jumla.
Kuchangia alau euro 250,000 kwenye miradi ya kitamaduni au euro 500,000 katika utafiti wa kisayansi - au kuunda nafasi 10 za ajira - pia kunaweza kusaidia kupata visa ya dhahabu. Waombaji lazima waruhusu ukaguzi wa rekodi za uhalifu na waonyeshe kuwa hawana deni.
Lima wa Prime Legal anaamini kuwa mifuko zaidi itaundwa sasa kwa vile mali isiyohamishika si chaguo tena - na kwamba baadhi ya mifuko iliyopo itajielekeza mbali na mali - na kwamba michango kwa miradi ya kitamaduni itakuwa maarufu zaidi.
Soma pia: BERLIN : Serikali ya Schroeder yapata pigo jipya la kashfa ya viza
Lakini Nuri Katz wa kampuni ya ushauri ya Apex Capital Partners alisema kutojumuisha uwekezaji wa mali isiyohamishika kutaifanya Ureno kuwa na mvuto mdogo kwa wawekezaji, ambao watageukia mipango ya viza za dhahabu ya nchi nyingine. Nchi jirani ya Uhispania ni miongoni mwa zile ambazo bado zinaruhusu uwekezaji katika majengo.
Katz alisema kuwa ukweli kwamba mifuko yenye vigezo inahitaji tu kuwekeza asilimia 60 ya pesa zao nchini Ureno kutapunguza zaidi manufaa ya mpango huo kwa taifa.
Wanasheria na makampuni ya ushauri kwa muda mrefu wamelalamika kuwa mchakato wa viza ni wa polepole na wa ukiritimba, na baadhi walitaka ufafanuzi zaidi kuhusu sheria mpya, ambazo zinazuia uwekezaji wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja wa mali isiyohamishika.
Wakili Raquel Cuba Martins alisema baadhi ya wateja wake pia walikuwa na wasiwasi kuhusu hatari ya kisiasa. Ureno itafanya uchaguzi wa mapema mwezi Machi baada ya serikali kusambaratika kufuatia msururu wa kashfa.
"Tayari tumepokea maombi ya kujiondoa kwa sababu ya ukosefu wa utulivu na uhakika", alisema Martins na kuongeza kuwa wengine sasa wanapendelea kuanza sasa mchakato kuliko kusubiri mabadiliko yanayoweza kufanywa na serikali mpya.