Mpinzani wa rais Putin yuko mahututi
20 Agosti 2020Alexei Navalny amelazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi baada ya kuzimia akisadiwa na mashine ya kupumua.
Alexei Navalny,mkosoaji mkubwa wa muda mrefu wa rais Vladmir Putin anapigania uhai wake hivi sasa baada ya kuugua akiwa kwenye ndege akisafiri kuelekea mjini Moscow kutoka mji wa Tomsk ulioko Siberia.
Msemaji wake aliyetowa taarifa hiyo leo asubuhi amesema Navalny mwenye umri wa miaka 44 aliugua kutokana na kile kinachoshukiwa kuwa sumu,na alipelekwa hospitali baada ya ndege aliyokuwemo kulazimika kutuwa kwa dharura katika eneo la Omsk.
Kira Yarmysh ameandika ujumbe kwenye ukurasa wa twita akisema Navalny amezimia na yuko katika hali mahututi.
Msemaji huyo wa Navalny pia aliiambia redio Echo Moskvy kwamba Navalny alikuwa akitokwa jasho jingi akiwa kwenye ndege na alimuomba amzungumzishe ili aweze kuendelea kuwa na fahamu ya kinachoendelea na baadae alikwenda msalani na kuzimia.
Huenda kiambata cha sumu kiliwekwa kwenye kimiminika
Yarmysh akaongeza kusema kwamba mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 44 ni lazima alikunywa kitu kilichotiwa ndani ya chai aliyokunywa mapema asubuhi alipokuwa katika mgahawa mmoja kwenye uwanja wa ndege kabla ya kupanda ndege hiyo.
Naibu mganga mkuu wa hospitali wa Omsk ambako anatibiwa mwanasiasa huyo Anatoliy Kalinichenko amewaambia waandishi habari kwamba Navalny yuko katika hali mahututi lakini iliyothibitiwa na madaktari wanafikiria kufanya vipimo mbali mbali ikiwemo cha kuangalia ikiwa sumu imehusika lakini pia alikataa kutowa maelezo zaidi kutokana na sheria inayomzuia daktari kutowa taarifa ya mgonjwa.
Hata hivyo katika ujumbe alioutowa msemaji wa mwanasiasa huyo mkosoaji wa rais Putin ameeleza kwamba madaktari wanasema sumu iliingia haraka kwenye mwili kutokana na kinywaji cha moto.
Itakumbukwa kwamba mwaka jana Navalny aliwahi kukimbizwa hospitali kutoka jela alikokuwa amefungwa baada ya kukamatwa na mamlaka na timu yake wakati huo pia ilisema ilishuku alipewa sumu.
Lakini madaktari baadae walisema alipata mzio au allergy mbaya na baada ya kutiwa alirudishwa jela siku iliyofuata. Ingawa pia kisa hiki kimekuja baada ya rais wa Belarus Alexander Lukashenko kudai wiki iliyopita kwamba Navalny anahusika kupanga maandamano ya umma dhidi ya kurudi tena kwake madarakani nchini humo ambayo yameshuhudiwa toka tarehe 9 Agosti.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Iddi Ssessanga