1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mpox yasambaa kwa kasi DR Congo

19 Agosti 2024

Zaidi ya visa 200 vya homa ya Monkeypox vimeripotiwa hadi sasa, katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4jde9
Maambukizi ya Mpox, DR Congo
Mtoto aliyeambukizwa Mpox, apata matibabu katika kituo cha Afya cha Nyiragongo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Picha: Zanem Nety Zaidi/Xinhua/IMAGO

Kati ya visa vilivyorekodiwa na kutibiwa, asilimia 75 ni watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 15, na wengi wa wagonjwa wanatoka katika kambi za wakimbizi zinazowahifadhi wahanga wa vita.

Huku Kongo ikiwa na zaidi ya asilimia 96 ya kesi za Monkeypox zilizoripotiwa duniani mwaka huu, nchi hiyo pia inakabiliwa na janga kubwa la kiafya, linalozidishwa na hali mbaya ya maisha katika kambi za wakimbizi.

Licha ya juhudi zinazofanyika kutoa elimu kwa umma, uhamasishaji bado ni mdogo kwenye maeneo yaliyoathirika.

Kongo, ambayo imerekodi zaidi ya asilimia 96 ya takriban kesi 17,000 za Monkeypox duniani mwaka huu, na vifo karibu 500 kutokana na ugonjwa huo, watu wengi walio katika hatari kubwa zaidi hawaelewi bado kuwepo kwa ugonjwa huo au kitisho kilichopo na kile kinachosababisha kuripuka kwa homa hiyo.

Soma pia: Sweden yatangaza kisa cha kwanza cha virusi hatari zaidi vya mpox

Katika kambi ya wakimbizi ya Bulengo, Sarah Bagheni, 35, anaonyesha dalili za Monkeypox, lakini hajui ni nini hasa.

Chanjo ya ugonjwa wa Homa ya Nyani imepatikana

''Nimeona vidonda vimeanza hapa mkononi na shingoni. Maji yanatoka kwenye vidonda hivi. Siendi popote, mimi ni mlemavu. Sijui nilikopata ugonjwa huu. Ninawashwa sana na sijisikii vizuri,' amesema Sarah Bagheni.

Inakadiriwa kuwa mamilioni ya watu hawapati msaada wa matibabu au ushauri katika eneo la mashariki mwa Kongo linalokumbwa na vita, ambapo makundi kadhaa ya waasi wanapambana na jeshi la Kongo kwa miaka mingi wakigombea maeneo yenye utajiri wa madini, na hivyo kusababisha mgogoro mkubwa wa wakimbizi.

Soma pia: Ugonjwa wa mpox watangazwa kuwa dharura ya afya ya umma

Hali katika kambi hizo ni mbaya na miundombinu ya matibabu haifikiki kwa urahisi. Mkuu wa kambi ya Bulengo, Mahoro Faustin alisisitiza kuwa hatuwa za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kuwafundisha wakimbizi kuhusu mbinu za kujikinga.

''Ilikuwa miezi mitatu iliyopita ambapo tulianza kuona watu katika kambi wakiwa na dalili za Mpox. Tangu wakati huo, hatujaweza kuthibitisha kama visa vimeongezeka. Baada ya kugundua, tuliwatahadharisha kuhusu ugonjwa huu hatari, lakini mpaka sasa, kwa kuwa hatujui njia ya maambukizi, tuna tatizo kubwa. Sote tuko kwenye hatari ya kuambukizwa," amesema Mahoro Faustin.

DR Kongo | Mpox (1997)
Ishara za maambukizi ya homa ya nyaniPicha: Brain WJ/BSIP/picture alliance

Soma pia: Hofu yatanda kufuatia mlipuko mpya wa homa ya nyani

Dokta Pierre Olivier Ngadjole, mshauri wa afya wa shirika la kimataifa nchini DRC, amesema kuwa takribani asilimia 70 ya visa vipya vya Monkeypox katika eneo la Goma katika miezi miwili iliyopita vilivyorekodiwa katika kituo cha matibabu kinachosimamiwa na Medair, vilitoka katika kambi za wakimbizi. Dokta Ngadjole amesema chanjo itakuwa chaguo bora zaidi la kutatua mgogoro huu.

Kulingana na Dr. Olivier, kuna hatari kubwa katika kambi za wakimbizi. "Ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia ya kugusana moja kwa moja, na katika kambi za wakimbizi, ambako kuna msongamano mkubwa, kuna watu wapatao 10 katika kila kaya. Tunajali sana kuhusu kuenea kwa ugonjwa huu. Chanjo ni dhamana kubwa kwa sababu ni ugonjwa ambao unaweza kuzuiliwa kwa chanjo.''

Ruth Alonga, DW, Goma.