Eneo lililozingirwa miezi 20 la Khartoum lapata msaada
28 Desemba 2024Sehemu ya mtandao wa kujitolea unaoratibu juhudi za msaada katika maeneo ya vita kwa taifa hilo imesema jumla ya malori 28 yaliwasili katika eneo la Jebel Awliya, kusini mwa Khartoum. Msafara huo ulijumuisha malori 22 yaliyokuwa yamebeba chakula kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), lori moja kutoka Shirika la Madaktari Wasio, na malori matano yaliyosheheni dawa kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF. Mashrika ya ndani na UNICEF wamesema vifaa hivyo vitasaidia kukidhi "mahitaji ya dharura ya afya na lishe ya watoto na familia zinazokadiriwa kufikia 200,000". Jebel Awliya ni moja kati ya maeneo mengi nchini Sudan yanayokabiliwa na njaa kubwa baada ya pande zinazozozana kuzuia barabara. Tangu vita vilipoanza Aprili 2023 kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya RSF, hakuna kilichoingia au kutoka bila idhini ya pande zote mbili.