Msafara wa misaada washambuliwa Syria
20 Septemba 2016Umoja wa Mtaifa umesema takriban magari 18 katika msafara wa magari 31 yameteketezwa hapo jana, yakiwa yanaelekea mji ulio vigumu kufikiwa wa Orum al-Kubra katiak jimbo la Allepo kuwasilisha misaada ya kiutu inayohitajika vibaya.
Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Syria lenye makaazi yake mjini London limesema wafanyakazi wa kujitolea wapatao 12 wa shirika la hilali nyekundu pamoja na madereva wao wameuawa katika mashambulizi hayo. Huku Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu Stephen O'Brian amesema iwapo mashambulizi hayo yatathibitishwa yalikuwa ya makusudi, basi yatahesabiwa kama uhalifu wa kivita.
Mtu ambaye hakujitambulisha kwa jina aliyevaa helmet jeupe na aliyenaswa katika mkanda wa vidio uliothibitishwa na shirika la habari la Reuters kuwa ni wakuaminika anaelezea hali ilivyo katika eneo la tukio.
"Hii ni ghala ya shirika la hilali nyekundu la Syria. Yalikuwepo magari 20, malori 20 yaliyojazwa chakula, unga na dawa, Pampers za watoto na mablanketi. Leo ni Septemba 19 ya mwaka 2016. Usiku saa 7:30 helikopta za serikali zililenga ghala hili kwa kutupa mabomu ya mapipa. Kituo cha ulinzi cha mji wa Urm kilituma gari la kubebea wagonjwa ili kuwaokoa waliojeruhiwa. Lakini serikali ilililenga eneo hili kwa mara nyengine," ameeleza mtu huyo.
Hakuna uthibitisho wa upande husika na mashambulizi
Shirika la kutetea Haki ta Binaaabu la Syria limesema haikuweza kuthibitisha iwapo ngede zulohusika na mashambulizi hayo ni za serikali ya Syria au za Urusi.
Msafara huo wa magari ulikuwa umebeba misaada ya kibinaadamu iliyokuwa ikitarajiwa kuwasaidia watu 78,000.
Mji wa mashariki wa Allepo ulioshikiliwa na waasi, wenye mamia kwa maelfu ya wakaazi, umekosa misaada ya kiutu tokea mwezi Julai, licha ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano ya hivi karibuni.
Mashambulizi hayo ya angani yalianza masaa machache baada ya jeshi la Syria kutangaza kumalizika kwa wiki moja ya kusitishwa mapigano yaliyosimamiwa na Marekani pamoja na Urusi. Jeshi la Urusi limesema haina maana kwa wanajeshi wa Syria kuzingatia makubaliano ya kusitisha mapigano huku wakiwa wanashambuliwa na wanamgambo.
Mashambulizi dhidi ya msafara wa magari ya misaada kwa hakika utaukasirisha vibaya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mtaifa unaoendelea mjini New York Marekani.
Wawakilishi kutoka Marekani, Urusi pamoja na nchi nyengine zinazohusika na mgogoro wa Syria, watakutana leo hii kwa mazungumzo ya kumaliza vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitano na kusababisha vifo vya watu wapatao 300,000 na wengine kadhaa kupoteza makaazi.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/rtre/dpae
Mhariri:Iddi Ssessanga