Msichana wa Kiroma ruksa kurudi Ufaransa
20 Oktoba 2013Kusafiririshwa kwa Leonarda Dibrani kumezusha shutuma nchini Ufaransa na kusababisha makundi makubwa ya wanafunzi kuingia barabarani wiki hii na kumuweka waziri mashuhuri wa mambo ya ndani Manuel Valls chini ya kiwingu cha shutuma.
Sehemu kubwa ya hasira kuhusiana na kurudishwa kwao kwa msichana huyo mwenye umri wa miaka 15 kulitokana na jinsi alivyotolewa kwa nguvu kwenye basi lililokuwa limejaa wanafunzi wa darasa lake wakati wa safari ya shule mapema mwezi huu kabla ya kusafirishwa kurudishwa kwao Kosovo pamoja na familia yake.
Hollande akizungumza hewani moja kwa moja na televisheni amesema iwapo msichana huyo atawasilisha ombi na kutaka kuendelea na masomo yake atakaribishwa lakini yeye tu.Hiyo ilikuwa ni kauli ya kwanza ya Hollande kuhusiana na kisa hicho ambacho kilikuja kuibuka hadharani hapo Jumatano.
Sheria ilifuatwa
Uchunguzi juu ya kurudishwa kwake Kosovo uliochapishwa Jumamosi umebaini kwamba hatua hiyo ilikuwa sahihi kwa mujibu wa sheria lakini polisi ingeliweza kutumia busara zaidi katika kutekeleza sheria hiyo.
Dibrani mwenyewe amelikataa pendekezo hilo la Hollande wakati akizungumza katika mji wa Mitrovica nchini Kosovo ambapo ndiko anakoishi na familia yake tokea kurudishwa kwao hapo Oktoba 9 kutoka mji wa mashariki wa Ufaransa wa Levier.
Amekaririwa akisema "Sitorudi Ufaransa peke yangu, sitoitelekeza familia yangu kwani sio mimi peke yangu ninayehitaji kwenda shule, kuna pia kaka zangu na dada zangu."
Baba yake Resat mwenye umri wa miaka 47 ameongeza kusema kwamba familia yake haitogawika na watarudi Ufaransa kwa njia yoyote ile. Amesema familia yake ilikuwa tayari imejumuika katika jamii ya Ufaransa na kwamba wataendelea kupigania hilo kwani watoto wake ni wageni huko Kosovo.
Dibrani wazazi wake na ndugu zake watano wa kiume na wa kike walikuwa wameishi Ufaransa kwa miaka minne wakati maombi yao ya kupatiwa hifadhi yakishughulikiwa kabla ya hatimae kukataliwa katika kipindi cha majira ya kiangazi.
Uchunguzi huo uliofanywa na wizara ya serikali umegunduwa kwamba polisi ilikwenda nyumbani kwa familia hiyo asubuhi ya tarehe 9 Oktoba ili kuisafirisha na kuirudisha kwao familia nzima lakini ili ilikuja kugunduwa kuwa msichana huyo alikuwa amelala kwenye nyumba ya rafiki yake kwa ajili ya safari hiyo ya shule.
Sheria za Ufaransa zinapiga marufuku hatua zozote za kuingilia kati vijana wadogo wakati wakiwa shuleni au karibu na maeneo ya shule.
Busara haikutumika
Repoti hiyo imegunduwa kwamba wakati basi hilo halikuwa karibu ya shule ya Dirbani polisi haikutanabahi hatari ya kuvuruga safari yake hiyo ya shule na haikuonyesha utambuzi unaohitajika.
Akitowa kauli yake hiyo iliyoonyeshwa kwenye televisheni Hollande amesema kuanzia sasa na kuendelea hatua za aina hiyo zitapigwa marufuku wakati wa saa za shule.
Matokeo ya uchunguzi huo yamezidi kumuimarisha Valls waziri wa mambo ya ndani ambaye umashuhuri wake umepindukia ule wa mkuu wake Hollande lakini alikuwa katika jicho kubwa la uchunguzi kutokana na kisa hicho.
Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kampuni ya BVA uliochapishwa leo katika gazeti la Le Parisian umeonyesha kwamba asilimia 74 ya wananchi wa Ufaransa wameunga mkono msimamo wa Valls.
Wakati watu wengi waliofanyiwa uchunguzi huo wa maoni ambao wanafikia kama 1,090 wenye umri wa miaka 18 na kupindukia wamesema walishtushwa na hatua ya kushikiliwa kwa Leornada asilimia 65 walikuwa dhidi ya kurudishwa Ufaransa kwa msichana huyo na familia yake.
Shinikizo la wanafunzi
Hata hivyo wanafuzi waliokuwa wakishiriki katika maandamano mjini Paris na katika miji mengine hapo Alhamisi na Ijumaa wamedai Dibrani na mwanafunzi mwengine Khatchik Kachatryan aliesafirishwa kurudishwa nchini kwao waruhusiwe kurudi Ufaransa kuendelea na masomo yao.
Kesi ya Dibrani imezidi kuwa ngumu baada ya kubainika kwamba baba yake alidanganya kuhusu familia hiyo kuwa na asili ya Kosovo ili kuweza kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuweza kupatiwa hifadhi nchini Ufaransa.
Katika mahojiano na AFP hapo Alhamisi Resat amesema ni yeye tu aliezaliwa Kosovo na kwamba mke wake na watoto wake watano kati ya sita akiwemo Leornada walikuwa wamezaliwa Italia.
Uchunguzi huo pia umegunduwa kwamba Leonarda na dada yake waliwahi kuchukuliwa na mashirika ya huduma za jamii baada ya kumtuhumu baba yao kwa kuhusika na matumizi ya nguvu dhidi yao madai ambayo baadae waliyatenguwa.
Utata wa kisa hiki unafuatiwa na shutuma zilizoibuka mwezi uliopita kufuatia kauli ya Valls ambapo amesema takriban watu wa kabila la Roma 20,000 walioko Ufaransa walikuwa hawana nia ya kujumuika katika jamii na walikuwa wanapaswa kurudishwa katika nchi walikotokea za asili.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Sudi Mnette