Msimamo wa Urusi Mashariki ya Kati na Afrika yatishia NATO
13 Machi 2022Lakini kwa uchunguzi mdogo wa kimataifa, Putin pia anashughulika na kuendeleza uwepo wa Urusi katika Mashariki ya Kati na Afrika, upanuzi ambao viongozi wa kijeshi na raia wanauona kama tishio jengine kwa usalama wa nchi za Magharibi.
soma Marekani, washirika wazidisha shinikizo la kiuchumi kwa Urusi
Mkakati wa Putin katika Mashariki ya Kati na Afrika umekuwa rahisi, na wenye mafanikio. Anatafuta ushirikiano wa kiulinzi na madikteta, viongozi wa mapinduzi, na wengine ambao wamepuuzwa au kudharauliwa na Marekani na Ulaya, ima kwa sababu ya ukiukaji wao wa umwagaji damu au kwa sababu ya maslahi kinzani ya kimkakati ya mataifa ya Magharibi.
Nchini Syria, waziri wa ulinzi wa Urusi mwezi uliopita alinadi ndege zenye uwezo wa kufanya mashambulizi ya nyuklia na makombora ya kisasa katika eneo la Mediterrania, kama sehemu ya ushirikiano wa kiusalama ambao sasa unaifanya Kremlin kutishia kutuma wapiganaji wa Syria nchini Ukraine.
Ushirikiano kwa maslahi gani?
Nchini Sudan, utawala wa kijeshi uliochukuwa madaraka katika taifa hilo la Afrika Mashariki ana muungano mpya wa kiuchumi na Kremlin, ushirikiano unaofufua ndoto za Urusi za kuwa na kituo cha jeshi la majini kwenye bahari ya Shamu.
Kulingana na maafisa wa Marekani Urusi pia hivi karibuni iliingia katika makubaliano ya ulinzi na Mali, ikiwa ya karibuni miongoni mwa mataifa ya Afrika yenye rasilimali nyingi kuunda ushirikiano wa kiusalama mamluki wenye mafungano na ikulu ya Kremlin.
Akizungumza na shirika la habari la The Associated Press Jenerali mstaafu wa Marekani Philip M. Breedlove ambaye aliwahi kuwa kamanda mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO kutoka 2013 hadi 2016, na sasa mwenyekiti mashuhuri katika taasisi ya utafiti juu juu ya masuala ya Mashariki ya Kati, amesema Urusi inajaribu kujionyesha kama dola kubwa, kama kiongozi katika masuala ya dunia, na kama inayoendesha mambo ya kimataifa.
Lakini wakati Putin akiwa tayari anapambana na upinzani mkali kutoka kwa jeshi dhaifu la Ukreine, wataalam wanaona malengo yake ya kujitanua katika Mashariki ya Kati na Afrika kama tishio la muda mrefu, sio hatari iliyopo kwa Ulaya au muungano wa NATO.
soma Urusi yaongeza mashambulizi katika miji ya Ukraine
Ili kufanikisha malengo yake ya kimkakati, Mara nyingi Urusi hutoa wanajeshi wa kawaida au mamluki wenye mafungamano na Kremlin kulinda tawala za viongozi waliotengwa. Badale yake, viongozi hawa huilipa Urusi kwa njia kadhaa, zikiwemo fedha taslimu au maliasili, ushawishi katika mambo yao, na kuunda misingi kwa ajili ya wapiganaji wa Urusi.
Miungano hii inasaidia kuendeleza malengo ya Putin ya kurejesha ushawishi wa Urusi katika mipaka yake ya enzi za Vita Baridi. Ushirika mpya wa kiusalama wa Urusi pia unaisaidia kidiplomasia.
Wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipolaani uvamizi wa Putin dhidi ya Ukraine mwezi huu, Syria ilijiunga na Urusi katika kupiga kura dhidi ya azimio hilo, na nyingi kati ya serikali za Kiafrika ambazo zimetia saini mikataba ya usalama na mamluki wa Urusi zilijizuwia.
soma Putin aamuru vikosi vya kujilinda viwe kwenye tahadhari
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock alisema katikati mwa Februari kwamba nchi za Magharibi hazingeweza tena kupuuza ushindani wa ushawishi kote barani Afrika, ambapo China inatumia mabilioni ya fedha katika miradi ya miundombinu kupata haki za madini, na Urusi hutoa usalama kupitia Mamluki wanaoungwa mkono na Kremlin.
Kuanzia 2015 hadi 2021, mamluki wa Urusi waliongeza uwepo wao kote ulimwenguni wakiendesha shughuli zao katika nchi 27
kwa mujibu wa Kituo cha Mikakati na Utafiti wa Kimataifa. Mamluki maarufu zaidi ni Kundi la Wagner, ambalo Marekani na Umoja Ulaya wanachukulia kama mbadala wa jeshi la Urusi, lakini Kremlin inakanusha hata kuwepo kwake.