1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Msuluhishaji wa mzozo wa Burundi amejiuzulu

Admin.WagnerD11 Juni 2015

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, Said Djinnit, amejiondoa leo hii kama msuluhishi katika mzozo wa kisiasa unaoikabili nchi hiyo, huku machafuko ya kirai yakiendelea kushuhudiwa.

https://p.dw.com/p/1FfIf
Afrika Said Djinnit Sonderbeauftragter UN
Picha: Getty Images/AFP/J.D. Kannah

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Burundi Said Djinnit, amejiondoa katika jukumu lake kama mpatanishi wa mazungumzo baina ya vyama vya siasa vinavyozozana pamoja na machafuko ya kiraia yanayoendelea kwa wiki kadhaa hadi sasa nchini humo.

"Said Djinnit amejiondoa katika nafasi yake kama msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, lakini atarejea tena Bujumbura kama mjumbe maalum wa kanda ya maziwa makuu," amesema Vladimir Monteiro, msemaji mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ujumbe wa Burundi.

Monteiro hata hivyo hakutoa sababu maalumu ya kujiondoa kwa Djinnit na wala Umoja wa Mataifa haukuweka wazi kama utamteua msuluhishaji mpya kwa Burundi.

Mapema wiki hii, viongozi wa mashirika ya kiraia na vyama vya upinzani walilalamika kuwa mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa alikuwa akielemea zaidi upande wa serikali, madai ambayo aliyapuuzilia mbali.

Burundi Proteste gegen Präsident Nkurunziza
Maandamano dhidi ya rais Pierre NkurunzizaPicha: Reuters/G. Tomasevic

Kiongozi wa asasi ya kiraia Vital Nshimirimana amesema itakuwa vyema kuchaguliwa msuluhishaji mpya ambaye hataelemea upande wowote, na kutoa wito kufanyike mazungumzo mengine ambayo alipendekeza yafanyike nje ya nchi.

Burundi imekuwa katika mgogoro wa kisiasa tangu mwezi wa Aprili mwaka huu baada ya rais Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kutaka kugombea urais kwa awamu ya tatu mfululizo, jambo ambalo limepingwa na raia pamoja na upinzani ukisema ni kinyume na katiba pamoja na makubaliano ya Arusha ya mwaka 2006 yaliyovimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 13.

Kiasi cha watu 40 wameuwawa katika operesheni ya polisi kuyakandamiza maandamo ya raia katika mji mkuu Bujumbura na takriban watu 100,000 wamekimbilia nchi jirani.

Baada ya jaribio la mapinduzi la mwezi uliopita Nkurunziza anakabiliana na shinikizo kubwa la kimataifa ikiwamo kuzuiwa kwa misaada ili kumshinikiza aachane na azma yake ya kugombea awamu ya tatu, jambo ambalo wanadiplomasia wanahofia litaitumbukiza tena nchi hiyo katika vita.

Wakati haya yakiarifiwa, waziri wa Maendeleo wa Ujerumani Gerd Müller, amesema Burundi inaelekea katika vurugu kwa sababu serikali inapuuza kanuni za kidemokrasia na hivyo Ujerumaji itasitisha shughuli zote za misaada kwa serikali ya Nkurunziza.

Licha ya upinzani mkali dhidi ya rais Nkurunziza kugombea urais kwa mara ya tatu, uchaguzi umepangwa kuendelea huku uchaguzi wa bunge ukitarajiwa kufanyika tarehe 26 Juni ukifwatiwa na wa rais tarehe 15 Julai.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/AFPE/RTRE/AFP

Mhariri:Josephat Charo