Msumbiji yaanza kuhesabu kura
10 Oktoba 2024Shughuli ya kuhesabu kura ilianza muda mfupi baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa majira ya saa 12 jioni kwa saa za Msumbiji, huku matokeo ya awali yakitarajiwa kutolewa katika muda wa wiki mbili zijazo.
Viongozi wawili wakuu wa upinzani wameonya kuhusu udanganyifu katika uchaguzi huo kwenye taifa hilo la kusini mwa Afrika, linalokabiliwa na viwango vya juu vya umasikini na ghasia za wapiganaji wa jihadi katika eneo la kaskazini.
Soma zaidi: Uchaguzi Msumbiji: Je, upinzani una nafasi?
Rais anayeondoka madarakani, Filipe Nyusi, mwenye umri wa miaka 65, baada ya kumaliza muda wake wa mihula miwili kwa mujibu wa katiba, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu na wenye subira, baada ya siku nzima ya kupiga kura kupita bila kuripotiwa matukio makubwa.
Akizungumza Jumatano baada ya kupiga kura Rais Nyusi alisema anaomba pasiwepo na kundi lolote la wananchi litakalowachokoza wengine na kuwatisha. ''Naomba kila kitu kifanyike kwa amani na utulivu. Tunapaswa kujiepusha kutangaza matokeo mapema sana, ndiyo maana tunatakiwa kuwa makini ili tusiuyumbishe mchakato Mzima,'' alifafanua Nyusi.
Mchakato wa uchaguzi wakosolewa
Kwa upande wake Venancio Mondlane, anayesimama kama mgombea binafsi ameukosoa mchakato mzima, akiielezea Tume ya Uchaguzi kama watu wala rushwa, wezi, na walaghai.
Akizungumza baada ya kupiga kura yake, Mondlane aliwaambia waandishi habari kuwa anaamini katika mchakato wa uchaguzi, lakini sio watu waliotumwa kuusimamia uchaguzi.
Mondlane amekuwa mpinzani mkubwa wa mgombea wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo, mwenye umri wa miaka 47, ambaye anapewa nafasi kubwa ya kushinda.
Mondlane na wagombea wengine wawili, Ossufo Momade, aliyekuwa kamanda wa waasi, na kiongozi wa chama kidogo cha upinzani, Lutero Simango, wameelezea wasiwasi wao kuhusu haki katika uchaguzi, wakidai miongoni mwa mambo mengine, masanduku ya kupigia kura yalikuwa yamefunguliwa kabla shughuli ya kupiga kura haijamalizika, na kwamba baadhi ya mawakala wao walinyimwa kibali cha kufuatilia upigaji kura.
Upinzani: Tunataka uchaguzi wa haki
Simango wa chama cha Mozambique Democratic Movement, MDM, amesema hatua ya kukataa kukabidhi vitambulisho kwa mawakala wa MDM kunaonesha ishara ya kuwepo udanganyifu. ''Leo, kile tunachokitaka ni kuuona mchakato huu unakuwa wa haki na uwazi,'' alisisitiza Simango.
Uchaguzi uliopita wa urais nchini Msumbiji uliofanyika mwaka 2019, ambao chama cha Frelimo kilishinda kwa asilimia 73 ya kura, uligubikwa na dosari, huku uchaguzi wa manispaa wa mwaka 2023 ukimalizika kwa ghasia baada ya matokeo kupingwa na upinzani.
(AFP, AP)