Wasiwasi umetanda Msumbiji, Mondlane aitisha maandamano
23 Desemba 2024Umma wa Msumbiji unasubiri kwa hamu uamuzi wa baraza la katiba kuhusu matokeo ya uchaguzi wa rais, yaliyozusha mvutano mkubwa.
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane ameapa kuamsha vurugu nchini humo, ikiwa baraza hilo litamthibitisha mgombea wa chama tawala, Daniel Chapo kuwa mshindi.
Wasiwasi umetanda nchi nzima
Wasiwasi umetanda kote nchini Msumbiji, huku macho yakielekezwa kwa Baraza la Katiba ambako majaji wanatarajiwa adhuhuri ya leo kutoa maamuzi waliyofikia kuhusu hatma ya matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Oktoba 9 yaliyompa ushindi mgombea wa chama tawala cha Frelimo, Daniel Chapo.
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane anadai,uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu na matokeo yaliyotangazwa na tume, yalichakachuliwa kumpendelea mgombea huyo wa Frelimo.
Anasema matokeo ya kura zilizohesababiwa na upande wake zinaonesha alishinda kura za kutosha kumpa ushindi wa kutwaa madaraka, na hivyo ndivyo anavyodhamiria kufanya.
Mondlane ambaye hayuko nchini Msumbiji, lakini anawaongoza wafuasi wake akiwa nje ya nchi, ametoa vitisho kwamba nchi hiyo itatumbukia kwenye vurugu ikiwa Baraza la Katiba haitotangaza kile anachosema ni matokeo halali.
Kupitia ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, siku ya Jumamosi aliwaambia wafuasi wake hivi, tunanukuu.
''Baadhi ya watu walifikiri hatua ya upinzani ya kuyapinga matokeo ni porojo, au masikhara, sasa watapata mshangao Januari 15 watakaponiaona Venancio Mondlane ninachukuwa madaraka, Maputo''
Mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mtangazaji wa kituo cha redio mjini Maputo, anasema maamuzi yatakayotolewa na baraza la katiba yataamuwa, ama kuipeleka Msumbiji kwenye hatma ya utulivu na amani au kuitumbukiza kwenye vurugu.Soma pia: Mkutano wa SADC utamudu kumaliza mzozo wa Msumbiji?
Ameapa kuanzisha kile alichokiita harakati za vuguvugu jipya la mapambano ambalo halijawahi kuonekana nchini humo.
Nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika imekuwa kwenye hali ya machafuko tangu tume ya uchaguzi ilipotangaza matokeo mnamo mwezi Oktoba yaliyompa ushindi mgombea wa Frelimo, chama kinachoshikilia madarakani tangu Msumbiji ilipopata uhuru kutoka kwa Wareno, mwaka 1975.
Rais wa sasa Fillipe Nyusi anakamilisha muda wake madarakani Januari 15 ambapo anatarajiwa kuyakabidhi madaraka kwa kiongozi mpya aliyechaguliwa.
Venancio Mondlane aendesha upinzani akiwa nje ya nchi
Hivi sasa Mondlane mwenye umri wa miaka 50 na anayevutia vijana wengi wa Msumbiji alikimbilia uhamishoni tangu alipouwawa wakili wake Oktoba 19, katika tukio analodai lilifanywa na vikosi vya usalama vya Msumbiji, na bado haijafahamika ikiwa anadhamiria kurejea.
Mvutano huu wa matokeo ya uchaguzi nchini humo umesababisha kushuhudiwa maandamano makubwa yaliyotatiza shughuli katika miji ya taifa hilo, kuhujumu shughuli za viwanda na mitambo ya umeme huku pia yakizuia shughuli za kwenye mpaka kati ya Msumbiji na Afrika Kusini, na kupelekea nchi hiyo jirani kupata hasara kubwa katika shughuli za usafirishaji.Soma Pia: Viongozi wa Afrika Kusini, Zimbabwe na Tanzania kuijadili Msumbiji
Tayari takriban watu 130 wameuwawa kwa mujibu wa Amnesty International.
Na kutokana na maandamano yaliyoitishwa leo na Mondlane na hali ilivyo, serikali ya Marekani imeongeza tahadhari kwa raia wake dhidi ya kuelekea Msumbiji huku kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis,jana Jumapili
akitowa mwito wa kufanyika mazungumzo ya maridhiano na nia njema kuondowa hali ya kutoaminiana nchini Msumbiji.
Mchambuzi mmoja wa kisiasa aliyeko Maputo Johann Smith anasema kinachoshuhudiwa Msumbiji ni sawa na hali iliyoshuhudiwa katika mataifa ya Kaskazini mwa Afrika mnamo mwaka 2010,akiyaita matukio ya Msumbiji ni Vuguvugu la mapambano Kusini mwa Afrika.