Mudavadi na Ruto waungana kabla ya uchaguzi mkuu Kenya
26 Januari 2022Mkutano wa kwanza wa vyama vya UDA, ANC na Ford Kenya umefanyika jijini Nakuru siku chache baada ya vigogo wa vyama hivyo kutangaza kwamba watashirikiana katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakaofanyika mwezi Agosti. Naibu Rais Wiliam Ruto ameiidhinisha hii kama mwanzo wa safari ya kuwa na serikali ya Rais wa tano wa Kenya.
Mkutano huo uliosubiriwa kwa hamu na kuhudhuriwa na umati mkubwa, umefananishwa na mkataba wa kisiasa kati ya Rais Uhuru Kenyata na naibu wake Ruto ulioidhinishwa mjini Nakuru mwaka 2013, jiji la Nakuru likiandikisha historia tena kama muhimu katika kutoa mwelekeo wa siasa za kitaifa.
Soma pia : Siasa za Kenya zachukua mkondo mpya kuelekea uchaguzi Mkuu
Ipi hatma ya muungano wa OKA ?
Chama cha UDA kinalenga kujipatia umaarufu katika sehemu zote nchini baada ya kukosolewa kwa kuzingatia maeneo ya mlima Kenya na bonde la ufa pekee ambayo ni ngome ya naibu Rais Ruto. Hatua ya Kinara wa ANC Musalia Mudavadi kuwahepa washirika wake wa muungano wa OKA na kuungana na naibu Rais Ruto imepiga jeki azma ya Urais ya Ruto ambaye alikuwa ameonekana kutengwa ndani na nje ya serikali. Akizungumza kwenye mkutano wa leo Mudavadi amewajibu waliomkosoa na kumuita msaliti kwa hatua aliyochukua.
Soma pia : Muungano mpya wa siasa wazinduliwa nchini Kenya
Mwanahabari mashuhuri Njogu wa Njoroge anayewania ubunge na mmiliki wa kampuni ya mvinyo ya Keroche Tabitha Karanja anayewania kiti cha useneta ni kati ya wafuasi wapya waliotambulishwa kujiunga na chama cha UDA.