Mugabe akaidi miito inayomtaka kujiuzulu
20 Novemba 2017Mugabe aliyehutubia taifa kwa njia ya televisheni, huku akikwama mara kwa mara, amesema ''Chama tawala, ZANU-PF kitakuwa na mkutano mkuu mwezi Desemba na nitauongoza mchakato huo.''
Kauli yake hiyo imeiingiza Zimbabwe katika sintofahamu kubwa, kwa sababu inaashiria kuwa anataka kuendelea kuwa rais hadi angalau katikati mwa Desemba.
Hiyo ni kinyume na matarajio ya raia wengi ambao walijimwaga mitaani mwishoni mwa juma lililopita kumshinikiza Mugabe mwenye umri wa miaka 93 kuachia ngazi, baada ya kuiongoza Zimbabwe kwa miaka 37.
Chama chake cha ZANU-PF ambacho muda wote kimesimama naye bega kwa bega, kilikuwa kimefanya kikao Jumapili, na kumfukuza kiongozi huyo katika wadhifa wa ukatibu mkuu, na kumpa muda wa hadi leo mchana kuwa amejiuzulu urais, la sivyo, hatua za kisheria zitumiwe kumshurutisha kuondoka madarakani.
Afumbia macho hali halisi
Katika hotuba yake Mugabe hakusema chochote kuhusu miito inayomtaka kujiuzulu, na amepuuza hatua ya jeshi kuchukua udhibiti wa nchi wiki iliyopita akisema ''haikutengua utaratibu wa kikatiba wala kuondoa mamlaka yangu kama mkuu wa nchi na Amiri Mkuu wa Jeshi''
Badala yake amezungumza kana kwamba hakuna kilichotokea, akitoa rai ya utulivu na mshikamano.
Matamshi ya Robert Mugabe na ukaidi wake vimewakasirisha Wazimbabwe wengi, na kuibua wasiwasi kwamba nchi hiyo inaweza kutumbukia katika ghasia na mivutano ya kisiasa.
Mkuu wa shirika la maveterani wa vita ambalo lina ushawishi mkubwa katika siasa za Zimbabwe, Chris Mutsvangwa ametaka maandamano mapya na hatua za kisheria kumshinikiza Mugabe kuondoka.
Mnangagwa (Mamba) awekwa katika nafasi nzuri kumpiku Mugabe
Baada ya kumfukuza Mugabe, chama cha ZANU-PF, kilimteuwa aliyekuwa Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa kuwa kiongozi wake mpya.
Derek Matyszak, mchambuzi wa masuala ya siasa aliyeko mjini Johannesburg amesema ukaidi wa Mugabe ni kama kujifurahisha na kujihadaa mwenyewe. ''Mkuu wa jeshi aliyekuwa pamoja naye alionekana kukerwa sana, na tumeshuhudia kwamba hakupiga makofi baada ya hotuba ya Mugabe,'' amesema Matyszak na kuongeza kuwa kinachofuata bila shaka ni utaratibu wa kisheria kumfungisha virago Mugabe.
Jeshi lilichukua udhibiti juma lililopita baada ya Mugabe kumfukuza kazi makamu wake Emmerson Mnangagwa, hali iliyodhihirisha kuwa alikuwa akitaka kumrithisha madaraka mkewe, Grace Ntombizodwa Mugabe.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,rtre
Mhariri: Caro Robi