Mugabe kuzikwa kwenye makaburi ya mashujaa
13 Septemba 2019Msemaji wa familia ya Mugabe Leo Mugabe, ameyathibitisha hayo mbele ya waandishi habari akisema kuwa machifu wa kikabila katika eneo alikozaliwa Mugabe ndiyo wameufikia uamuzi huo. Leo ambaye ni mpwa wa Mugabe amesema mazishi hayo yatakuwa ya kifamilia na wanaendelea kujadiliana zaidi kuhusu siku atakayozikwa kiongozi huyo wa zamani wa Zimbabwe.
''Kama wamesema uamuzi wao kwamba atazikwa katika makaburi ya mashujaa wa kitaifa, sasa tunachohitaji kufanya ni kusubiri taarifa zaidi. Nadhani ni muhimu kuangalia kama mazishi yatakuwa ya kifamilia au ya umma. Nadhani suala la mazishi ya kifamilia lilikuwa mjadala mkuu wa machifu. Hivyo nahitaji kupata uthibitisho kutoka kwao, kuangalia jinsi mchakato unavyoendelea hadi sasa,'' alifafanua Leo.
Mvutano kati ya familia na serikali
Familia ya Mugabe na serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa, mshirika wa zamani wa Mugabe ambaye aligeuka na kuwa mpinzani wake, zimekuwa katika mvutano kuhusu eneo atakalozikwa Mugabe. Serikali ya Mnangagwa, ilipendekeza Mugabe azikwe kwenye makaburi ya mashujaa wa kitaifa mjini Harare, huku familia yake ikitaka Mugabe azikwe katika shughuli ya kifamilia, kwenye kijiji chake cha Kutama, kaskazini magharibi mwa mji mkuu Harare.
Kwa sasa mwili wa Mugabe uko katika uwanja wa michezo wa Harare na watu wanaendelea kutoa heshima zao za mwisho. Watu kadhaa walijeruhiwa jana baada ya kukanyagana wakati waombolezaji waliokuwa kwenye foleni kusukumana wakitaka kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa kiongozi huyo wa zamani wa Zimbabwe.
Viongozi wa kimataifa kushiriki maziko ya kimataifa
Viongozi mbalimbali wa kimataifa wanatarajiwa kuanza kuwasili Ijumaa mjini Harare kabla ya maziko ya kitaifa yaliyopangwa kufanyika siku ya Jumamosi katika uwanja wa taifa wa michezo.
Rais wa China, Xi Jinping, kiongozi wa zamani wa Cuba, Raul Castro pamoja na marais kadhaa wa Afrika, akiwemo wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na Uhuru Kenyatta wa Kenya, ni miongoni mwa viongozi wa kimataifa watakaohudhuria mazishi ya Mugabe siku ya Jumamosi mjini Harare.
Mugabe alifariki dunia nchini Singapore wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 95. Aliiongoza Zimbabwe kwa miaka 37, kabla ya jeshi kumlazimisha kuondoka madarakani mwishoni mwa mwaka 2017. Mwili wake ulirejea Zimbabwe siku ya Jumatano.
(AFP, AP, Reuters)