Museveni ashinda uchaguzi Uganda
20 Februari 2016Kwa mujibu wa matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Jumamosi (20.02.2016)mpinzani akiyemkaribia Museveni ambaye ni kiongozi wa upinzani Kizza Besigye wa chama cha Mabadiliko ya Demokrasia MDC amejipatia asilimia 35.
Besigye mwenyewe yuko katika kifungo cha nyumbani wakati Museveni akitangazwa mshindi huku polisi wakiwa na silaha nzito wameweka ulinzi karibu na nyumbani kwa Besigye katika viunga vya mji mkuu wa Kampala.
Chama tawala cha Museveni NRM kimewahimiza wagombea wote kuheshimu matakwa ya wananchi na mamlaka ya tume ya uchaguzi na kukubali matokeo.Chama hicho kimetowa taarifa muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo ikisema "Tunawataka Waganda wote kuwa watulivu na wenye amani na kutofanya vurugu zote zote zile."
Hata hivyo chama cha upinzani cha Besigye kimewasihi Waganda wote na jamii ya kimataifa kuukataa na kulani udanganyifu huo wa uchaguzi ambao ulikua bayana kabisa.
Kura alizopata Museveni
Badru Kigundu akimtangaza mgombea wa chama cha NRM kuwa mshindi amesema kapata kura 5,617,503 sawa na aslimia 60.75 ya kura 9,246,563.Dr Kiza Besigye ambaye hii ni mara ya nne kushindwa na kushikilia nafasi ya pili amepata kura 3,270,290 sawa na asilimia 35 huku aliyekuwa waziri wa zamani.
Amama Mbabazi akipata kura 132,574. Ijapokuwa kuna matokeo ya vituo fulani ambayo hayajawasilishwa, lakini hata idadi ya wapiga kura wote katika kituo hicho ikiongezwa kwa idadi ya Dr. Besigye hawezi kumfikia Museveni.
Ijapokuwa hali imebaki tulivu, kuna taharuki kubwa jijini Kampala ambapo kwa kauli za baadhi ya watu imetokana na hatua ya polisi kumweka mgombea wa FDC katika kizuizi cha nyumbani pamoja na kuimarishwa kwa doria katika sehemu zote. Mpinzani huyo mkuu wa rais Museveni alikamatwa hapo jana kwenye makao makuu ya chama hicho katika operesheni ambapo hata helikopta zilitumiwa kuwasambaratisha wafuasi wa chama hicho.
Akizungumzia kisa hicho, Naibu msemaji wa polisi Polly Namaye alifafanua kwamba Besigye na wenzake walikuwa wanapanga kujitangaza washindi kwa mujibu wa matokeo ya wawakilishi wao.
Mazingira ya kutisha
Polisi haijatoa tamko rasmi kuhusu kizuizi hicho cha nyumbani na kwa kuwa mitandao ya kijamii imefungwa watu walioko ndani nyumbani kwa Besigye hawawezi kuwasiliana na walioko nje kufahamishana kuhusu tukio hilo.Hadi wakati wa kwenda hewani polisi walikuwa wangali wameyazingira makazi ya mgombea Dr. Kiza Besigye na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia au kutoka na kila aliyejaribu kuzungumza na wanahabari kwa mfano meya wa jiji la Kampala Erias Lukwago alikamatwa na kuzuiliwa kwenye kituo jirani cha polisi cha kasangati.
Kiongozi wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya Eduard Kukan amewaambia waandishi Jumamosi kwamba uchaguzi ulikuwa na "mazingira ya vitisho ambayo kwa kiasi kikubwa wahusika walikuwa maafisa wa vyombo vya dola.
Kwa mujibu wa repoti ya awali ya Umoja wa Ulaya wafuasi wa upinzani walinyanyaswa na na maafisa wa polisi katika wilaya zaidi ya 20.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Lubega Emmanuel