Museveni kuwakutanisha Warundi Uganda
28 Desemba 2015Mazungumzo hayo katika Ikulu ya rais mjini Entebbe nje ya mji mkuu wa Uganda Kampala yatasimamiwa na rais Yoweri Museveni aliyeteuliwa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa mpatanishi.
Naibu Waziri wa mambo ya nchi za nje Henry Oryem Okello aliliambia gazeti la serikali New vision kwamba, kile ambacho Uganda inataka ni kuona aina zote za mauaji yanayoendelea Burundi yatasitishwa mara moja.
Machafuko nchini Burundi yalianza mwezi Aprili, baada ya rais Pierre Nkurunziza kutangaza azma yake kugombea mhula wa tatu ambapo aliendelea na mpango huo na kushinda uchaguzi mwezi Julai uliosusiwa na vyama vya upinzani.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Burundi Alain-Aime Nyamitwe anauongoza ujumbe wa serikali, ambapo wajumbe wa upinzani ni pamoja na wanachama wa muungano wa CNARED unaoongozwa na Leonard Nyangoma.
Kwa upande wake muungano huo unasisitiza kwamba unafuata makubaliano ya amani ya Arusha yaliofikiwa 2006 na kumaliza vita vya zaidi ya miaka 10 vya wenyewe kwa wenyewe na unasema mhula wa tatu wa Nkurunziza unahujumu makubaliano hayo. Wajumbe wa asasi za kiraia akiwemo mwanaharakati Pierre-Claver Mbonimpa pamoja na viongozi wa kidini pia wanashiriki.
Marekani yasema Museveni hana muda
Kwa mujibu wa Katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nchi za nje anayemaliza muda wake James Mugume, mazungumzo hayo yatajadili ajenda kabla ya kuanza majadiliana hasa.
Kwa upande mwengine Marekani ilisema wiki iliopita kwamba rais Museveni hana muda wa kupatanisha kwa sababu ameshughulika na kampeni za uchaguzi utakaofanyika mwezi uajo ambapo yeye binafsi ni mgombea tena Urais.
Watu wapatao 240 wameuawa katika miezi kadhaa ya machafuko mitaani na hasa mji mkuu Bujumbura, kukiweko na mashambulizi ya mara kwa mara ya watu wenye silaha na mapigano ya risasi nyakati za usiku na kila siku kukikutikana maiti katika barabra za mji mkuu huo. Wengine 200,000 wameikimbia nchi hiyo.
Umoja wa Afrika wenye wanachama 54 umesema utatuma kikosi cha wanajeshi wapatao 5,000 kuzuwia machafuko licha ya serikali ya Burundi kukiita kikosi hicho kuwa cha , “uvamizi”. Pia baada ya Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kupendekeza mbele ya Baraza la Usalama la Umoja huo, kutumwa kikosi cha Umoja wa mataifa nchini Burundi, serikali ya nchi hiyo ilisema hakukuwa na haja ya kutumwa kikosi cha aina hiyo nchini humo.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/ afp, Daily Monitor (Uganda)
Mhariri: Mohammed Khelef