1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni lazima aimarishe haki za binadamu

12 Mei 2021

Shirika la kuteta haki za Binaadam la Amnesty International limemtaka Rais Yoweri Museveni wa Uganda kutumia muhula wake mpya kubadili hali inayoendelea ya kuzorota kwa haki za binadamu nchini humo.

https://p.dw.com/p/3tI4v
Jahresbericht von Amnesty International
Picha: Monika Skolimowska/dpa/picture alliance

Museveni alitangazwa mshindi kwa jumla ya asilimia 58.6 ya kura Januari mwaka huu, mbele ya mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine ambaye alipata asilimia 34.8 kulingana na tume ya Uchaguzi. Matokeo ambayo Kyagulanyi aliyapinga na kuwasilisha kesi mahakamani. Soma zaidiMuseveni aapishwa kwa muhula wa sita madarakani

Uchaguzi wa Uganda ulifanyika baada kampeni zilizoghubikwa na ukiukwaji wa haki za binaadam ikiwa ni pamoja na mauwaji ya kinyume cha sheria, kukamatwa kiholela kwa viongozi na wafuasi wa upinzani, na kushambuliwa kwa waandishi wa habari.

Serikali ilikiri kuhusika na mauwaji

Uganda | Präsident Yoweri Museveni
Picha: Luke Dray/Getty Images

Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Africa Deprose Muchena amesema, Serikali ya Uganda ilikiri kuwa maafisa wa usalama waliwapiga risasi na kuwauwa watu wasiopungua 54 mnamo Novemba 2020 kujibu maandamano yaliyoenea juu ya kukamatwa kwa Robert Kyagulanyi, alipokuwa kwenye harakati za kampeni. Waathiriwa wa maandamano hayo bado hawajapata haki, ukweli wala fidia. Soma zaidi Bobi Wine awasilisha mahakamani rufaa iliyorekebishwa

Wafuasi na viongozi wengi wa upinzani waliokamtwa kiholela bado wapo kizuizini na wanateswa gerezani. Wengine wengi wamewekwa kizuizini bila kujulikana, wakati wengine wameshtakiwa katika korti za jeshi licha ya kwamba wao ni raia, hali inayokiuka viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Amnesty International inasema, Mamlaka ya Uganda lazima imuachilie mtu yeyote aliyewekwa kizuizini, mara moja na bila masharti kwa sababu ya kutekeleza haki zao za kibinadamu kwa amani.

Watetezi wa haki katika shinikizo

Uganda Kampala mit Schnellfeuergewehr bewaffnete Polizisten Passant Wahlplakate
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Watetezi wa haki za binadamu pia wamewekwa chini ya shinikizo kubwa katika miezi ya hivi karibuni, na wengine walibandikiziwa mashtaka ya jinai ya uwongo, akiwemo Nicholas Opiyo mwanaharakati wa kutetea haki za binaadam ambaye anaendelea kupambana na kesi ya ubadhirifu wa fedha pamoja na wengine wanne.

Mtandao wa Haki za Binadamu kwa Wanahabari nchini Uganda (HNRJ) uliripoti zaidi ya kesi 100 za ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya waandishi wa habari wakati wa kampeni za uchaguzi, pamoja na kesi za vurugu za polisi, hasa wakati wakiripoti kuhusu wagombea wa kisiasa. soma zaidi Bunge la Uganda lalaani ukandamizaji wakati wa uchaguzi

Muchena amesema matukio ya mauaji haramu, kupigwa, kutekwa nyara, kuwekwa kizuizini kiholela na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu na vikosi vya usalama vya Uganda kabla, wakati na baada ya uchaguzi hayapaswi kufumbiwa macho. Rais Museveni lazima atumie muhula wake wa sasa kuiongoza Uganda katika mustakabali wa kuheshimu haki za binadamu.

Ili kufanikisha hili itahitaji kuchunguza ukiukaji huu na mwengine wa awali juu ya haki za binadamu, kuhakikisha kuwa wale wote wanaoshukiwa kuhusika kufikishwa mahakamani, na kwa haki kulipa fidia wahasiriwa na familia zao kwa mateso waliyopitia.

Chanzo/Amnesty International