1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini yaendelea kufifia

Admin.WagnerD17 Juni 2015

Wasiwasi unazidi kuwa mkubwa juu ya mustakabali wa sarafu ya Euro baada ya Waziri wa fedha wa Ujerumani kusema hana matumaini juu ya kupatikana suluhisho la mgogoro wa Ugiriki kwenye mazungumzo ya mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/1Fig3
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: REUTERS/Alkis Konstantinidis

Waziri wa fedha wa Ujerumani Schäuble aliwaambia wabunge wa nchi yake leo kwamba hakuna matayarisho yoyote yaliyofanyika juu ya kufikia uamuzi kwenye mkutano wa mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro. Kauli ya Waziri Schäuble imenukuliwa na mbunge mmoja ambae hakutaka kutajwa.

Schäuble amesema hana matumaini iwapo pande tatu zinazoidai Ugiriki zitakubaliana na nchi hiyo juu ya kuipa fedha nyingine ili kuiokoa .

Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras amesema leo kwamba madai yanayotolewa na pande tatu zilizoikopesha Ugiriki ya kuitaka iyakate mafao ya uzeeni, hayaeleweki. Waziri Mkuu wa Ugiriki pia ametahadharisha ,kwamba ikiwa mazungumzo juu ya kuiokoa nchi yake yatashindikana Ulaya yote itaathirika.

Waziri Mkuu wa Ugiriki Tsipras ameitoa kauli hiyo wakati ambapo Benki kuu ya nchi yake pia imetahadharisha juu ya madhara makubwa ya kiuchumi yanayoweza kutokea , ikiwa suluhisho halitapatikana mnamo wiki hii.

Matumaini yafifia

Mawaziri wa fedha wa nchi za ukanda wa sarafu ya Euro wanatarajiwa kukutana kesho mjini Brussels. Pande tatu zinazoidai Ugiriki zilikuwa matumaini ya kupatikana suluhisho kwenye mkutano wa hapo kesho. Lakini matumaini hayo yamefifia mnamo wiki hii kutokana na Ugiriki na wadai wake kutafautiana juu ya mageuzi ambayo Ugiriki inalazimika kuyafanya ili ipatiwe mikopo zaidi.

Wasi wasi umezidi kuwa mkubwa ,kwamba huenda makubaliano yasipatikane hadi mwishoni mwa mwezi huu ambapo, mpango wa kuiokoa Ugiriki unafikia mwisho, wakati nchi hiyo inapaswa kulilipa shirika la fedha la kimataifa,IMF kiasi cha Euro Bilioni 1.6

Merkel asisitiza matumaini

Hata hivyo kauli ya matumaini imetolewa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Amesema anadhamiria kufanya kila litakalowezekana ili Ugiriki iendelee kuwamo katika ukanda wa safaru ya Euro.

Mazungumzo yamethibiti kuwa magumu baina ya Ugiriki na pande tatu zilizoikopesha nchi hiyo, Shirika la Fedha la Kimataifa,Benki Kuu ya Ulaya na Umoja wa Ulaya. Waziri Mkuu wa Ugiriki Tsipras amesema nchi yake imejitahidi kupiga hatua kwa kadri ilivyoweza ili kuyatekeleza masharti yaliyotolewa na pande hizo tatu.

Wachambuzi wametahadharisha kwamba, ikiwa Ugiriki itashindwa kuyalipa madeni yake na hivyo kujitoa kwenye Euro, Umoja wa Ulaya utaathirika kwa kiwango kikubwa sana.

Mwandishi: Mtullya Abdu/afpe/ZA

Mhariri: Mohammed Khelef