Mutharika rais mpya Malawi
1 Juni 2014Mutharika ambaye ni ndugu wa rais Bingu wa Mutharika aliyefariki wakati akiwa madarakani hapo mwaka 2012, amewataka wagombea wengine 11 wa urais kuungana naye kuijenga upya nchi hiyo baada ya baadhi yao akiwemo Banda kuyapinga matokeo ya uchaguzi huo hapo awali.
Akiungana na Makamo wa Rais Saulos Chilima kula kiapo mbele ya jaji mkuu,Mutharika amesema anajihisi kuwa "mnyenyekevu sana " kuwa rais wa tano wa taifa hilo la kimaskini kusini mwa Afrika.
Mutharika amesema katika hotuba yake ya kwanza tokea alipotangazwa kuwa rais hapo Ijumaa "Ni dhahir kwamba tunakabiliana na matatizo makubwa katika nchi hii.Sote kwa pamoja tujenge nchi hii ambayo iko kwenye ukingo kwa kusambaratika."
Akikubali kushindwa mapema Jumamosi,Banda amempongeza Mutharika kwa ushindi wake huo uliokuwa na mchuano mkali.
Matokeo ya uchaguzi
Matokeo ya uchaguzi huo wa tarahe 20 Mei yalitangazwa Ijumaa dakika chache baada ya mahakama kuu kukataa jaribio la dakika za mwisho kuzuwiya kutolewa kwa matokeo hayo na kutowa nafasi ya kuhesabiwa upya kwa kura.
Tume ya uchaguzi imesema Mutharika amejipatia asilimia 36.4 ya kura dhidi ya asilimia 20.2 alizopata Banda na mkuu wa tume huyo Maxon Mbendera kumtangaza Mutharika "rais mteule".
Matokeo hayo yameonyesha Banda kushika nafasi ya tatu katika kinyan'ganyiro hicho baada ya Lazarus Chakwera wa chama cha Malawi Congress(MCP) kushika nafasi ya pili kwa kujipatia asilimia 27.8 ya kura.
Msemaji wa chama hicho Jessie Kabwila ameliambia shirika la habari la AFP kwamba chama hicho cha MCP kitayapinga matokeo hayo mahakamani.
Banda ataka Mutharika asaidiwe
Banda ambaye amekuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Malawi hapo mwaka 2012 alitaka uchaguzi huo utangazwe kuwa "batili na haufai" kwa hoja kwamba ulikuwa na hitilafu nyingi.
Lakini hakutaja suala la udanganyifu wakati alipotowa taarifa yake akikubali kushindwa na ameitaka nchi hiyo kumsaidia Mutharika.
Amesema anataka kuwahimiza wananchi wote wa Malawi kumuunga mkono rais mpya aliyechaguliwa Malawi Profesa Mutharika na serikali yake wakati wakishughulikia msingi wa maendeleo na kufanya juhudi za kuiendeleza zaidi Malawi.
Banda ameuelezea uchaguzi huo kuwa ulikuwa na mvutano na kutaja matokeo ya hapa na pale ya vurugu. Mtu mmoja aliuwawa wakati polisi walipofyetuwa gesi ya kutowa machozi na risasi za mpira kwa waandamanaji waliokuwa wakidai kuhesabiwa upya kwa kura katika mji wa kusini mashariki wa Mangochi.
Lakini ameongeza kusema kwamba Wamalawi wanapaswa kusonga mbele kama taifa moja kuendelea kuungana, kudumisha utawala wa sheria na kuendelea kuwa watu wa amani na utulivu wakati wakielekea kipindi kengine cha miaka hamsini ya mustakbali wa Malawi.
Kinga ya kutoshtakiwa
Mutharika anachukuwa hatamu za kuiongoza nchi hiyo wakati akikabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 74 anatuhumiwa kwa kujaribu kuficha kifo cha kaka yake akiwa madarakani miaka miwili iliopita katika harakati za kumzuwiya Banda wakati huo akiwa makamo wa rais kushika madaraka.
Banda alifanikiwa kuchukuwa madaraka ya rais kama inavyoamuriwa na katiba na kumtimuwa Mutharika kutoka katika serikali wakati huo akiwa waziri wa mambo ya nje.
Mutharika ambaye ni profesa wa sheria na waziri wa zamani anakabiliwa na mashtaka mengine ya ziada ya kuchochea uasi na kula njama ya jinai kwa kushirikiana na maafisa wengine.
Kesi hiyo bado imekwama lakini wachambuzi wanasema yumkini kesi hiyo ikawekwa kando kutokana na kwamba marais wa Malawi wanakuwa na kinga ya kutoshtakiwa kwa kadri wanapokuwa madarakani.
Kuna tetesi kwamba mara tu baada ya Mutharika kuingia madarakani anaweza kumgeuzia kibao Banda kwa kumfungulia mashtaka ya rushwa ya kashfa iliopachikwa jina "cashgate" yenye kuhusisha zaidi ya dola milioni 30.
Banda amedai kupatiwa sifa kwa kuibuwa kashfa hiyo ambapo fedha za misaada zimemezwa kwenye mifuko ya maafisa waandamizi wa serikali.Lakini wakosoaji wake akiwemo Mutharika wanasema fedha hizo zimetumika katika kampeni ya uchaguzi ya chama chake.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri : Amina Abubakar