Mvutano India na Pakistan waongezeka
30 Septemba 2016India na Pakistan zimewahi kupigana mara mbili kuhusu jimbo hilo la Kashmir, huku kila upande ukidhibiti sehemu ya jimbo hilo. India imechukua hatua ya mapema kwa kuwaondoa wanakijiji wake zaidi ya elfu 10 wanaoishi karibu na mpaka wa Pakistan. Waziri mkuu Narendra Modi aliviagiza vyombo vya usalama kuimarisha doria katika majimbo ya Jammu na Kashmir ambayo ni sehemu ya kilomita elfu 3,300 ya mpaka kati ya mataifa hayo jirani yenye uwezo mkubwa wa zana za kinuklia. India ilichukua hatua hiyo ya kuwahamisha raia wake baada ya kutangaza kufanya mashambulizi katika eneo la mpaka la kashmir linaloshikiliwa na Pakistan, dhidi ya wapiganaji wanaoshukiwa walikuwa wakijitayarisha kutekeleza mashambulizi nchini India.
Pakistan yashtumu mashambulizi ya India
Hata hivyo serikali ya Pakistan kupitia waziri wake wa maswala ya kigeni Mohammed Zakaria imeyalaani mashambulizi hayo na India. "Katika muda wa siku 83 zilizopita.Majeshi ya India yamewaua zaidi ya wakashimir waislamu wasiokuwa na hatia 100 wakiwemo watoto, akinamama na vijana. Pia yamewajeruhi macho zaidi ya watu 800 kwa kutumia bunduki marisao, mamia kupofuka kabisa na wengine kuwa na uwezo wa kuona kidogo. Zaidi ya watu elfu 12 pia wamejeruhiwa," alisema waziri huyo.
Mzozo kati ya Pakistan na India umeendelea kwa miaka mingi ambapo mara kwa mara wamekuwa wakishambuliana. Balozi wa Pakistan katika umoja wa mataifa Maleeha Lodhi amesema taifa lake linautaka umoja wa mataifa kuingilia kati mgogoro wa sasa ili kutuliza hali.
Mwanajeshi wa India atekwa
Taarifa nyingine ni kuwa majeshi ya Pakistan yametangaza kumteka mwanajeshi wa India ambae alivuka mpaka unaodhibitiwa na mataifa hayo mawili, saa chache baada ya wanajeshi hao kushambuliana kwa risasi.
Hata hivyo India imesema mwanajeshi huyo alivuka eneo hilo bila kukusudia na atarejea nyumbani baada ya mashauri ya kijeshi.Taharuki kati ya majirani hao ilizuka mapema mwezi huu baada ya wapiganaji kuvamia kambi ya majeshi ya India eneo la Kashmiri na kuwaua 19 miongoni mwao. New Delhi inadai wapiganaji hao wanaendesha shughuli zao nchini Pakistan.
Mara zote India imekuwa ikipinga vikali maazimio yanayotolewa na Umoja wa Mataifa yanayotaja kwamba Kashmir ni sehemu ya Pakistan. Mgogoro wa Kashmiri ulianza mwaka 1947 wakati wa kugawanywa Bara Hindi. Pakistan inaamini, Umoja wa Mataifa una wajibu wa kuheshimu maazimio yake na kuilazimisha India nayo iheshimu maazimio hayo hususan suala la kupewa haki wananchi Waislamu wa Kashmiri ya kujiamulia wenyewe mustakbali wao.
Mwandishi: Jane Nyingi/RTRE/DPAE
Mhariri: Yusuf Saumu