1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvutano kuhusu hijabu nchini Uturuki

7 Februari 2008

Bunge la Uturuki katika kikao cha kwanza kilichodumu zaidi ya saa 13 limepiga kura kufanya mageuzi ya Katiba ili kuweza kuondosha amri inayowazuia wanafunzi wa kike kuvaa hijabu katika vyuo vikuu.

https://p.dw.com/p/D3lD

Wabunge 404 kutoka jumla ya 550 wameunga mkono pendekezo la kubadilisha Katiba ya Uturuki na 92 wamepinga na hivyo theluthi mbili inayohitajiwa imepatikana.Hata hivyo mswada huo uliopendekezwa juma lililopita na chama tawala cha Waziri Mkuu Tayyip Erdogan cha AKP na chama cha upinzani cha kizalendo MHP,unahitaji kupigiwa kura tena katika duru ya pili Jumamosi ijayo ikitazamiwa kuwa utapita bila ya shida kwani bungeni,vyama hivyo viwili vina wingi uliopindukia theluthi mbili.

Mageuzi hayo lakini yanapingwa vikali na makundi ya wasomi ikiwa ni pamoja na majemadari jeshini,majaji na wakuu wa vyuo vikuu.Wao wanasema,kuondosha amri inayopiga marufuku kuvaa hijabu katika vyuo vikuu,kutadhoofisha msimamo wa serikali unaotenganisha masuala ya kisiasa na dini - msingi mmojawapo mkuu wa jamhuri ya kisasa ya Uturuki.

Mbunge mmoja wa chama cha upinzani CHP,Nur Serter amekituhumu chama tawala AKP kuwa kinatumia vibaya hisia za kidini.Mbunge huyo wa kike amesema,vazi la hijabu linasababisha mgawanyo nchini na kuwafanya wanawake kama raia wa tabaka ya pili.Wapinzani wa mageuzi hayo wana hofu kuwa serikali,pole pole inataka kuifanya Uturuki nchi inayotumia sheria za Kiislamu kama ilivyo katika nchi ya jirani Iran.

Lakini Waziri Mkuu Erdogan ameahidi kuwa serikali itaheshimu sera ya kutenganisha masuala ya kisiasa na dini. Akaongezea kuwa wanafunzi wa kike wanaotaka kujifunika kichwa wasinyimwe haki ya kupata elimu ya juu kwa sababu ya kuvaa hijabu.Amesem,anataka kuruhusu vazi la hijabu kwenye vyuo vikuu ili kuimarisha uhuru wa dini na kibinafsi. Theluthi mbili ya wanawake nchini Uturuki hutumia vazi la kujifunika kichwa na wengi walisita kuendelea na masomo yao katika vyuo vikuu baada ya amri iliyopiga vazi la hijabu katika taasisi za umma,kuviingiza vyuo vikuu katika kundi hilo mnamo mwaka 1989.

Siku ya Jumamosi,zaidi ya raia 120,000 wanaiotaka serikali ifuate sera ya kutenganisha masuala ya kisiasa na dini, waliandama katika mji mkuu Ankara na miji mingine nchini humo,kupinga mpango wa serikali.Na kiongozi mmoja wa chama kikuu cha upinzani Deniz Beykal ametishia kuishtaki serikali katika Mahakama ya Katiba.