Mwanadiplomasia wa Ufaransa ahimiza utulivu Lebanon
28 Aprili 2024Mwanadiplomasia mkuu wa Ufaransa Stephane Sejourne, ametoa wito wa utulivu nchini Lebanon wakati wa ziara yake ya pili tangu kulipozuka mvutano wa mashambulizi ya kuvuka mpaka na Israel yaliyochochewa na vita vya Gaza.
Sejourne alitembelea makao makuu ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon UNFIL na kusisitiza kwamba Paris inahimiza uepushaji vita nchini humo.
Israel na kundi la Hezbollah la nchini Lebanon linaloungwa mkono na Iran, zimekuwa zikishambuliana kwa kufyatiliana risasi karibu kila siku tangu shambulizi la Hamas dhidi ya Israel Oktoba 7.
Mapigano yameongezeka katika wiki za hivi karibuni, huku Israel ikipiga hatua zaidi ndani ya ardhi ya Lebanon, huku Hezbollah ikiongeza mashambulizi yake ya makombora na ndege zisizo na rubani kwenye maeneo ya kijeshi kaskazini mwa Israel.