Mwanamfalme Harry na Markle wafunga ndoa
19 Mei 2018Mwanamfalme Harry amemuoa Meghan Markle katika sherehe kubwa leo Jumamosi katika kanisa la Kifalme la Mtakatifu George ndani ya kasri la Windsor. Mamilioni ya watazamaji katika televisheni duniani kote wamefuatilia sherehe hiyo sambamba na wageni chungunzima mashuhuri walihudhuria.
Harry alijumuika na kaka yake na ambaye ni msaidizi wake wa karibu katika harusi hiyo, mwanamfalme William , mwenye umri wa miaka 35, wakati mama yake Markle mwenye umri wa miaka 62, Doria Ragland, akiongozana nae. Markle alivalia shela jeupe lililotengenezwa na kampuni ya kifaransa iliyoko London ya Givenchy. Kofia zilitawala sherehe hiyo huku mama harusi Doria Ragland akiwa amevalia suti ya rangi ya kijani na kutupia kofia yake. Wageni pia wakiwemo Oprah Winfrey na Stella McCatney walitupia kofia za rangi ya pinki zilizorandana vizuri na nguo walizovalia.Ndoa hiyo ilifungishwa na kiongozi mkuu wa kanisa la Anglikana la Uingereza askofu mkuu wa Canterburry Justin Welby.
Harusi hiyo inatajwa kwamba ilikuwa ya mvuto wa kipkee ya kifalme ikilinganishwa na ya Kate Middleton aliyeolewa na mwanamlfame William mwaka 2011 ambapo aliyeangaziwa zaidi kwenye harusi hiyo alikuwa dada wa Kate Middleton Pippa Middleton.
Viongozi mbali mbali duniani wametuma pongezi kwa wanandoa hao wapya katika ufalme wa Uingereza akiwemo waziri mkuu wa Canad Justin Treudeu. Miongoni mwa wageni 600 waalikwa ni pamoja na waliowahi kuwa wapenzi wa Harry Cressida Bonas alivalia kigauni cha michoro cha rangi ya pinki kijani na njano huku mpenzi mwengine wa zamani wa Harry Chelsy Davy akitokea na kigauni kifupi cha rangi ya buluu ya kuiva au (Navy Blue)mradi kila aliyehudhuria harusi hiyo alipendeza kivyake.
Tukio hilo la harusi lililochukua muda wa saa moja lilifuatiwa na msafara wa dakika 20 nje ya kasri katika gari la kukokotwa na farasi.
Baba wa bi harusi hakuhudhuria harusi hiyo. Thomas Markle, mwenye umri wa miaka 73, alifanyiwa upasuaji wa moyo siku ya Jumatano.
Harry na Markle wamewakaribisha mamia ya watu kushuhudia sherehe hizo katika viwanja vya kasri la kifalme, wakati mamia kwa maelfu ya watu wanaosherehekea harusi hiyo wakijipanga katika njia ilikopita gari ya kukokotwa na farasi.
Polisi imepiga marufuku kurusha maua na mapambo wakati wa msafara huo , wakielezea kuhusu wasi wasi wa usalama. Wageni waalikwa wanajumuika katika sherehe maalum ya kula na kunywa pamoja na Prince Harry na mkewe Markle ambapo vyakula mbali mbali vimeandaliwa kwa ajili ya wageni hao.
Uingereza imekuwa ikivutia dunia kwa harusi za kifalme, matukio ya sherehe za kuvutia na haiba ambayo inasababisha mvuto kwa familia ya kifalme.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri:Caro Robi